Apandishwa kizimbani kwa Kumtisha Rais Magufuli Kupitia WatsApp
Mfanyabiasha Leonard Materu (31) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka ya kutuma ujumbe wa kumtishia Rais John Magufuli kupitia mtandao wa WhatsApp.
Materu ambaye ni mkazi wa Moshi Bar Kwadiwani, alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka yake na Wakili wa Serikali, Diana Lukondo mbele ya Hakimu Mkazi Magreth Bankika.
Akisoma mashitaka Wakili Diana alidai, mshitakiwa huyo amefunguliwa kesi hiyo ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa WhatsApp chini ya Sheria ya Mtandao ya mwaka 2015.
Ilidaiwa kuwa, Julai 17, mwaka huu jijini Dar es Salaam, Materu aliandika ujumbe wenye lengo la kudanganya umma kupitia WhatsApp ukisomeka; “Magu ajiandae tunaenda kupindua mpaka Ikulu.”
Inadaiwa kuwa maneno hayo yalikuwa na lengo la kumtishia Rais John Magufuli. Baada ya kusomewa mashitaka, mshitakiwa alikana kutenda kosa hilo, na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Mshitakiwa aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja alisaini hati ya Sh milioni tano. Kesi itatajwa tena Septemba 20, mwaka huu.