Majibu ya Waziri Mkuu Kuhusu Mauaji ya Askari na Uchumi wa Nchi ,Bungeni leo

DODOMA:
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kukutana na wadau tofauti wanaohusika na masuala ya uchumi katika kuhakikisha uchumi wa nchi unaendelea kukua.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim, Majaliwa alipokuwa akijibu swali la
Mbunge wa Hai Mhe. Freeman Mbowe mijini Dodoma aliyetaka kujua hali ya uchumi ilivyo kwa sasa hapa nchini.
Waziri Mkuu  amesema kuwa lengo kuu la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha uchumi wa nchi unaongezeka kupitia nyanja tofauti kwa kushirikiana na taasisi za fedha zilizopo ili kufikia uchumi wa kati kama ilivyoanishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
Akizungumza kuhusu suala la midororo wa upokeaji wa mizigo katika bandari nchini, Waziri Mkuu amesema kuwa mdororo huo umetokana na kupungua kwa kiasi cha mizigo na  kushuka kwa uchumi duniani.
Katika suala ya mauaji yaliyotokea Tanga, Mwanza na Vikindu, Waziri Mkuu amesema kuwa usalama wa wananchi utaendelea kuimarishwa huku serikali ikiahidi kupambana vitendo vya mauaji kwa raia na askari katika maeneo mbali mbali nchini.
 
“Serikali imesikitika sana na jambo hili la mauaji hivyo itahakikisha wauaji hao wanawekwa katika mikono ya Sheria na kuongeza ulinzi kwa maeneo yote nchini kwa kuanzia ngazi ya vitongoji” alifafanua Waziri Mkuu.
Mbali na hayo Waziri Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya dola katika kuthibiti matukio hayo.
Kuhusu suala la uwepo wa tozo katika zao la korosho swali limeibuliwa na Mbunge wa viti maalumu Mhe.Riziki Lulida (CUF), Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Serikali imeshatoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia uondoaji wa Tozo zisizo na maana katika zao la korosho