RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, leo amewaongoza waumini wa Kiislamu katika kusherehekea sikukuu ya Eid El Hajj ambayo ni maarufu kama ‘Eid ya Kuchinja’




RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, leo amewaongoza waumini wa Kiislamu katika kusherehekea sikukuu ya Eid El Hajj ambayo ni maarufu kama ‘Eid ya Kuchinja’.
Hafla hiyo imefanyika jijini Dar es Salaam kwenye viwanja vya makao makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Kinondoni, jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 1:30 asubuhi ambapo Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa na Mufti Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi, na viongozi wengine wamehudhuria sherehe hizo.
Akizungumza katika viwanja hivyo, Zuberi amesema kuwa anawatakia Waislamu kote nchini na wananchi kwa jumla sikukuu njema ya Eid El Hajj ili kila mmoja aisherehekee kwa utulivu na mshikamano.
Amewataka pia walimu kote nchini wa shule za Kiislamu za madrasa kufanya jitihada kubwa ya kuhakikisha wanawaelimisha wanafunzi wao ili waweze kuwa na maadili mema ya dini yao na akaongeza kuwa kazi yao si kuwapatia elimu ya dini yao tu, bali wafundishwe pia masomo mbalimbali na lugha za nchi nyingine ili kuwawezesha kuwa na maadili mema na utaalam unaotakiwa katika maisha yao ya baadaye na kuwa viongozi bora.
Naye Mzee Mwinyi amesisitiza suala la amani kwa Watanzania wote huku akikazia maneno ya Mufti Zuberi aliyokuwa ameyatamka ili waumini waweze kubadilika akimaanisha kuondokana na dhana zote potofu zisizokuwa na manufaa katika kulijenga taifa.







Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Suleiman Lolila, akitoa mawaidha.
NA DENIS MTIMA/GPL