Sanamu mbili mpya za kiongozi wa muda mrefu wa Zimbabwe Robert Mugabe zimezinduliwa mjini Harare na kuzua utata mkubwa

Sanamu mbili mpya za kiongozi wa muda mrefu wa Zimbabwe Robert Mugabe zimezinduliwa mjini Harare.
Sanamu hizo, ambazo zilizinduliwa katika ikulu ya rais zimetayarishwa na mchongaji sanamu maarufu Dominic Benhura.
Rais Mugabe ameeleza kufurahishwa na sanamu hizo mbili kwa mujibu wa gazeti la serikali The Herald.


    "Hii ni kazi nzuri Sanaa ya Sanaa na wasanii walioshiriki inaonekana wana vipaji adimu, wana vipaji kwa kweli," amenukuliwa Bw Mugabe.
    Bw Benhura ameoneshwa kwenye picha zilizochapishwa na gazeti la The Herald akiwa amesimama karibu na sanamu hiyo akiwa na Bw Mugabe na mke wa rais Dkt Grace Mugabe.
    Sanamu hiyo, ambayo urefu wake ni karibu maradufu kimo cha Rais Mugabe, inamuonesha kiongozi huyo wa umri wa miaka 92 akiwa na miwani yake maarufu, masharubu na akiwa ameinua mkono akiwa ameufumbata kama ngumi.
    Baadhi ya raia nchini Zimbabwe hata hivyo hawajapendezwa na sanamu hizo na wanasema zinaonekana kama vibonzo.
    "Robert Mugabe ametukanwa kwa sanamu hii na bado hajaelewa," mmiliki wa gazeti ambaye pia ni mwanaharakati Trevor Ncube ameandika kwenye Twitter.
    "Ningelikuwa Robert Mugabe yule mtawala wa kiimla, ningeamuru (Benhura) akamatwe na niue sanamu hizo."