Tangazo kwa Wanafunzi waliofadhiliwa mafunzo ya uzamili 2016-17

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO

                          TAARIFA KWA UMMA 
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anawatangazia wafuatao kuwa wamepata ufadhili wa kugharamiwa mafunzo yao ya Uzamili/Uzamivu kwa mwaka wa masomo 2016/2017. Ufadhili huu utahusu malipo ya ada na posho ya utafiti tu kwa waliopata ufadhili wa “Basket Fund”ndani ya nchi na kwa wale waliopata ufadhili wa “Global Fund” watalipiwa ada, posho ya kujikimu (stipend), na posho ya vitabu na ya utafiti pamoja na wale waliopata ufadhili nje ya nchi. Malipo ya posho yatalipwa kwa kuzingatia viwango vilivyopitishwa na Wizara. Wizara haihusiki na malipo ya pango la nyumba au bweni kwa mwanafunzi aliyepata ufadhili hilo ni jukumu lake mwanafunzi. Ufadhili huu unahusu wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa masomo ambao watagharamiwa kwa kipindi chote cha masomo. Watumishi hawa waliochaguliwa wanatakiwa kujaza mkataba wa makubaliano ya ufadhili (bonding agreement) na Wizara kabla ya kuanza masomo yao. Aidha, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inasisitiza kuwa haitahusika kugharamia mafunzo ya mwanafunzi yeyote atakayeamua kujiunga na masomo katika chuo chochote kwa mwaka 2016/2017 ambaye hayuko kwenye orodha hii au mwanafunzi yeyote ambaye yuko kwenye orodha hii lakini hajajaza mkataba wa makubaliano ya ufadhili. Kila mtumishi aliyepata ufadhili atalazimika kuingia kwenye tovuti ya Wizara ya Afya ili kupata nakala ya mkataba ambao atatakiwa kujaza nakala tatu katika sehemu zinazomhusu na sehemu ya “guarantor” wa kwanza atajaza mwajiri wake au yeyote mwenye mamlaka ya kusaini kwa niaba ya mwajiri wake na “guarantor” wa pili anapaswa kuwa mtu yeyote mwenye sifa za kuingia mkataba kwa mujibu wa sheria za nchi. Mikataba hiyo (nakala tatu) ikikamilika kujazwa itawasilishwa Wizarani pamoja na picha 3 (passport size) na mwanafunzi husika ili Wizara iweze kukamilisha kusaini mikataba hiyo. Mwisho wa kuwasilisha mikataba hiyo ni tarehe 15/12/2016. Mkataba wa makubaliano ya ufadhili (bonding agreement) unapatikana kwenye tovuti ya Wizara www.moh.go.tz 

Imetolewa na; 
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto