Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ,awapa ahueni walimu waliotoa kipigo

BAADA ya uamuzi wa kuwafukuza vyuo walimu wanne waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo katika Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Mbeya (Mbeya Day), serikali imesema vyuo husika vinaweza kushauri adhabu mbadala iwapo vitajiridhisha kuwepo kwa mazingira tofauti na yaliyozingatiwa kwenye uamuzi wa kuwafukuza vyuo.


Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema hayo juzi alipozungumza na waandishi wa habari mkoani Mbeya alikokuwa katika ziara kwenye shule mbalimbali mkoani humo.

Profesa Ndalichako alisema uamuzi uliochukuliwa na ofisi yake ulizingatia sheria ndogo zilizotungwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) zinazoainisha makosa yanayoweza kumfukuzisha chuo mwanafunzi.

Hata hivyo, alisema uamuzi uliochukuliwa unaweza kutazamwa upya na vyuo husika iwapo uzito uliochukuliwa na wizara utaonekana kuwa katika mazingira na uhalisia wa tukio husika.

Walimu wanne waliokuwa kwa vitendo katika shule ya Mbeya Day walifukuzwa vyuo baada ya uamuzi wa serikali kutokana na kuhusika kumpiga mwanafunzi Sebastain Chinguku vibao, mateke na fimbo kwa ukatili Septemba 28 mwaka huu shuleni humo.

Walimu hao walibainika baada ya kipande cha video kusambazwa katika mitandao ya kijamii hivi karibuni. Waliohusika na vyuo walivyokuwa wakisoma ni Frank Msigwa (anayedaiwa kumpiga zaidi mwanafunzi makofi kichwani), John Deo na Sante Gwamaka wote wa DUCE-UDSM, na Evans Sanga wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.