Idadi ya wanafunzi walio disco vyuo vikuu yaongezeka

WAKATI mjadala wa ubora wa elimu nchini ukiendelea kuibua mambo kila uchao, takwimu zinaonyesha kuwa kuna idadi kubwa inayoongezeka ya wanafunzi wanaotemwa vyuoni (discontinuation) maarufu ‘disco’ kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo za ufaulu hafifu usiokidhi vigezo vya chuo.


Uchunguzi uliofanyika ukihusisha mahojiano na viongozi wa masuala ya taaluma katika vyuo vikuu viwili vikubwa zaidi vya umma nchini vya Dar es Salaam (UDSM) na Dodoma (UDOM), umeonyesha kuwa mbali na ongezeko la wanafunzi wanaofungishwa virago kabla ya kumaliza masomo yao (disco), idadi ya wale wanaorudia mitihani yao maarufu kama ‘suppliments’ au ‘sup’ pia imekuwa ikiongezeka kila uchao katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.


Katika uchunguzi huo imebainika kuwa baadhi ya sababu za kuwapo kwa ongezeko hilo la wanafunzi wanaokumbana na ‘disco’ au kurudia mitihani hutokana na sababu nyingi, baadhi zikiwa ni ukata wa fedha za ada na matumizi pindi wanapocheleweshewa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB); utoro wa baadhi ya wanafunzi ambao mahudhurio yao kwenye vipindi darasani huwa ya kusuasua na pia kupungua kwa ari ya kujisomea waliyo nayo baadhi ya wanafunzi, ambao hutegemea zaidi vyanzo vya mitandao isiyo rasmi katika kujisomea kupitia ‘google’ badala ya kusoma vitabu rasmi kwa wingi.


Sababu nyingine ni pamoja na baadhi ya wanafunzi kujisahau na kujihusisha zaidi na starehe kwa kuchukulia kila siku kuwa ni kama wikiendi kwao.


Sababu zingine za kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaotemwa vyuoni na pia wanaorudia masomo yao zimebainika kuwa ni baadhi yao kutumia muda mwingi kujihusisha na mijadala ya kwenye makundi mbalimbali ya mitandao ya kijamii kama facebook, twitter na whatsapp; baadhi yao kulazimika kuacha masomo baada ya kupata ufadhili wa masomo katika maeneo mengine na pia wapo wanaoacha kwa sababu ya shinikizo la waajiri kwa wale wanaoingia vyuoni wakiwa wameajiriwa.


HALI ILIVYO UDSM, UDOM
Akizungumza ofisini kwake jana, Mkurugenzi wa Masomo ya Shahada ya Kwanza UDSM, Prof. Allen Mushi, alisema idadi ya wanafunzi wanaoachia masomo kwa sababu ya kufeli mitihani imekuwa haitabiriki kwa sababu hupanda na kushuka kwa vipindi tofauti.


Hata hivyo, Prof. Mushi alisema kuwa kwa ujumla, takwimu zinaonyesha kuwa wanafunzi hao wanaoachia ngazi (disco) zimekuwa zikipanda katika kipindi cha kuanzia mwaka wa masomo 2012/2013 hadi kufikia 2015/2016.


Prof. Mushi alisema mwaka wa masomo 2015/16, wanafunzi wa madarasa yote walioshindwa kuendelea na masomo (disco) kwa sababu mbalimbali ikiwamo kufeli ni 526 kati ya 23,044, idadi ambayo ni sawa na asilimia 2.3 ya wanafunzi wote wa mwaka huo.


Alisema katika kipindi cha mwaka wa masomo 2014/15, walioshindwa kumaliza masomo ni 322 kati ya 22,572 (asilimia 1.45) wakati mwaka uliotangulia wa 2013/14, wanafunzi walioshindwa kumaliza masomo wakiwa ni 301 kati ya 19,554, sawa na asilimia 1.54.


Alisema kwa mwaka wa masomo 2012/2013, wanafunzi walioshindwa kumaliza masomo yao walikuwa 244 kati ya 19,224, ambayo ni sawa na asilimia 1.27.


Akifafanua kuhusiana na wanafunzi hao waliokatiza masomo, Prof. Mushi alisema wako wa makundi makubwa matatu, ambayo ni la wale waliofeli mitihani kwa kushindwa kufikia ufaulu unaotakiwa; kundi la wale walioshindwa kufanya mitihani bila ya kutoa taarifa kwa uongozi wa chuo na kundi jingine ni lile wanaloliita kuwa la walioshindwa kwa sababu nyinginezo.


“Mbali na wanaofeli kabisa mitihani, wengine unakuta tu mtu kaamua kukaa huko aliko bila kutoa taarifa kama ana dharura au matatizo mbalimbali ya kifamilia, mwisho wa siku anajikuta anadisco (anashindwa kuendelea na masomo),” alisema Prof. Mushi na kuenongeza:


“Wengine wanashindwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kukiuka misingi na kanuni za kinidhamu anapokuwa chuoni hapa. Hawa nao wanaonekana kuongezeka katika kipindi hiki,” alisema.


Akitoa mfano kwa ambao ‘wamedisco’ kutokana na kutofanya mitihani huku wakiwa hawajatoa taarifa, Prof. Mushi alisema mwaka wa masomo wa 2012/13 walikuwa 44, mwaka 2013/14 walikuwa 44, mwaka 2014/15 walikuwa 37 na mwaka 2015/16 walikuwa 76.


Akielezea suala hilo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Idrisa Kikula, alisema wastani wa wanafunzi wanaofeli na kuachia masomo njiani kwa sababu mbalimbali kila mwaka katika chuo hicho ni asilimia 2.4.


Alitaja sababu zinazowafanya wafeli kuwa ni pamoja na matatizo ya kifamilia, ugonjwa bila kutoa taarifa kwa chuo na wengine ‘hudisco’ kutokana na kushindwa kufikia kiwango cha ufaulu cha GPA ya 1.6 au kukamatwa wakikiuka sheria za mitihani, ikiwamo kuibia na kufanya udanganyifu.


“Sababu zipo nyingi zinazowafanya wanafunzi kufeli… lakini kwa ujumla, kwa mchanganyiko huo kwa kila mwaka wanaofeli hapa (UDOM) huwa ni wastani wa asilimia 2.4,”alisema Prof. Kikula.


Prof. Kikula alitaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na wanafunzi kushindwa kulipa ada na wengine kupata ujauzito pasi na kutoa taarifa kwa chuo kama taratibu zinavyoelekeza.


“Kwa mfano, mtu akiugua kuna taratibu za kufuata ili kuahirisha mitihani yake. Sasa wengine hawatoi taarifa. Ikifika siku ya mtihani hakuna taarifa zake na hivyo anakuwa amediscountinue,” alisema Makamu Mkuu huyo na kuongeza:


“Kuna wanaopata GPA ndogo na kukata rufaa wasiporidhika… wanasahishiwa upya na wanaweza wakafaulu kupitia rufaa zao au yabaki maamuzi ya awali ya kudiscountinue…” alisema Prof. Kikula.


WANAORUDIA MITIHANI
Kutokana na takwimu zilizopo UDSM, inaonyesha kuwa kwa ujumla, idadi ya wanafunzi wanaorudia masomo huwa haitabiriki kwa sababu hupanda na kushuka.


Prof. Mushi alisema katika mwaka wa masomo 2012/13, wanafunzi waliorudia mitihani walikuwa 5,918 kati ya wanafunzi 19,624 waliofanya mitihani, idadi ambayo ni sawa na asilimia 30.16, mwaka 2013/14 walikuwa 4,871 kati ya 19,554 (asilimia 24.91), mwaka 2014/15 walikuwa 4,867 kati ya 22,572 waliofanya mitihani (asilimia 21.6) na mwaka 2015/2016 ni wanafunzi 6,567 kati ya wanafunzi 23,044 waliofanya mitihani, sawa na asilimia 28.5.


Alisema kwa taratibu za chuo, wanafunzi hupewa fursa ya kutosha ya kurudia mitihani waliyofanya vibaya ikiwa ni pamoja na kuwa na miaka miwili ya ziada ya muda wao wa masomo pindi inapobidi ili kujisahihisha kupitia utaratibu uitwao “carry over”.


Alisema katika mwaka wa masomo 2012/2013, wanafunzi walio ‘carry over’ masomo yao walikuwa 360, mwaka 2013/2014 walikuwa wanafunzi 475, mwaka 2014/2015 ni wanfunzi 441 na mwaka uliopita wa 2015/2016 walikuwa wanafunzi 719.


Prof. Mushi alisema hawajafanya utafiti ili kufahamu sababu za kuwapo kwa ongezeko la wanafunzi wengi kushindwa masomo yao (disco), lakini anaamini kuwa baadhi ya sababu ni pamoja na baadhi yao kubweteka baada ya kufika chuoni hapo, wengine ni matakwa ya waajiri wao ambao huwalazimu kuachia ngazi ili wasipoteze kazi zao na wengine ni kupata ‘scholarship’ pasi na kutoa taarifa za kuondoka kwao UDSM.


“Mpaka sasa hatujafanya utafiti rasmi unaoonyesha sababu hasa ni nini zinazowafanya wanafunzi washindwe kumaliza au kufeli mitihani yao.


Lakini kuna wengine baadhi ambao hufika hapa na kubweteka kwa kuvimba kichwa, wakifikiria kuwa watafaulu tu kwakuwa huko nyuma katika hatua zingine za elimu walifanya vizuri,” alisema.


Kuhusiana na hofu kuwa labda miundombinu yao haiendani na idadi kubwa ya wanafunzi walio nao na ndiyo maana baadhi hufeli, Prof. Mushi alisema hiyo siyo sababu kwakuwa chuo chao kina nafasi za kutosha na hakijawahi kudahili kwa asilimia 100 ya uwezo wake.


Kwa mfano, Prof. Mushi alisema mwaka huu wa masomo (2016/2017) chuo kilikuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 9,900 lakini waliopatikana ni 9,904 tu, hivyo kuwa na upungufu wa wanafunzi 806.


Alisema mwaka uliopita (2015/2016), alisema chuo kilikuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 9,740 lakini kilidahili wanafunzi 9, 217 tu.


WAHADHIRI, WANAFUNZI WANENA
Mhadhiri wa UDSM, Dk. Benson Bana, alisema kwa utafiti mdogo uliofanyika, wanafunzi wengi hawana ari ya kujisomea maktaba na kwamba wanatumia mitandao ya kijamii hasa kupitia google kwa ajili ya kusoma yale wananyofundishwa na ambayo wakati mwingine hupotoshwa na vyanzo visivyo rasmi.


Alisema sababu zingine ni wanafunzi kutoingia katika mihadhara chuoni hapo na kwamba wahadhiri kwa kuona wanafunzi hao ni watu wazima, hawana muda wa kuwafuatilia.


Benson Alex ambye ni mhadhiri katika Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya UDSM, alisema sababu nyingine ya kufanya vibaya kwa baadhi ya wanafunzi ni maandalizi ya msingi ya wanafunzi hao, hasa katika shule walizotoka.


Alisema kuna baadhi ya wananfunzi waliosoma katika shule za gharama ambazo zilikuwa zikiwapa kila kitu na kwamba hakuna utaratibu wa mwananfunzi kujituma kusoma vitabu zaidi ya kile anachopewa, jambo ambalo mwishowe huwagharimu.


Alisema utaratibu wa UDSM ni wa kumfanya mwananfunzi awe mtafutaji wa kile anachoelekezwa na mwalimu wake, lakini kutokana na msingi mbovu waliotoka nao, baadhi ya wanafunzi wanashindwa kuendana na utaratibu huo na kujikuta wanashindwa kuendelea na masomo.


“Sababu zingine ni msingi waliotoka nao wanafunzi hao. Kuna wanafunzi walisoma katika shule za gharama ambazo walikuwa wakipewa kila kitu, utaratibu wa chuo chetu ni kumpa mwanafunzi asilimia 25 na anatakiwa kutafuta zilizobaki,” alisema Benson.


Akizungumzia hali hiyo, Rais wa Serikali ya Wanafunzi UDSM, Erasmi Leon, alisema baadhi ya wanafunzi hawazingatii sheria za mitihani hasa zinazokataza kuingia na vitu ndani ya chumba cha mtihani zikiwamo simu na mwishowe hujikuta wakichukuliwa hatua zikiwamo za kufukuzwa chuo.


Aliongeza kuwa zipo pia sababu zingine za kimazingira ambazo ni pamoja na baadhi ya wanafunzi kushindwa kuzingatia ratiba na kufanya mambo ambayo hayajawapeleka chuoni.


Alisema kuna baadhi ya wanafunzi chuoni hapo wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na kuiga tabia wanazozikuta kwa wenzao na kujikuta wanasahau masomo na kufanya shughuli zingine, baadhi zikiwa kinyume cha maadili ya jamii.


“Kuna baadhi ya wanafunzi wanashindwa kuendelea na masomo kwa kuwa hawafuati ratiba na kile walichofuata, wengine kutokana na mazingira wanaiga wenzao wanaowakuta chuoni na mwishowe wanafeli kwa kujisahau,” alisema Leon.


Kadhalika, Leon alisema baadhi ya wanafunzi wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na kukosa ada ya chuo na fedha kwa ajili ya kujikimu, hasa pale mikopo inapochelewa.


Alisema changamoto nyingine ni kukosekana kwa makazi rafiki kwa wanafunzi.