Jinsi ya kuhifadhi pesa na kuwa mmoja wa watu matajiri duniani
Moja ya matatizo yanayowasumbua watu wengi sana ni jinsi ya kutunza fedha ya akiba. Wengi wetu tunapokuwa hatuna hela tunakuwa na mawazo mazuri sana na ukiona mtu anachezea hela unaona kama hana akili au hajielewi. Ila unapozipata hela akili yote inahama, mipango yako yote mizuri unaisahau na unajikuta unatumia tu hovyo mpaka zinaisha. Zikiisha unarudi tena kwenye mzunguko ule wa kupata mawazo mazuri ya kutekeleza utakapopata fedha.
Leo katika kona yetu ya ushauri tutazungumzia kuhusu kuweka akiba na kutoitumia kwenye matumizi mengine hasa ya starehe. Wasomaji wengi wameniandikia kuhusu swala hili wakiomba ushauri. Hapa naweka ujumbe wa msomaji mmoja kama alivyoniandikia;
ninashindwa kutunza pesa nayoipata, nikiwa nina pesa kwenye acount kama mshahara wangu nashindwa kuishi kwa amani mpaka pesa iishe kabisa, afu zikiisha naanza kujuta tena, cjui nifanyeje..
Tatizo analokutana na msomaji huyu kuna watanzania wengi sana wanaokutana nalo na huenda wewe ni mmoja wao. Leo nataka tushauriane ni jinsi gani unaweza kuondokana na tatizo hili ili uweze kuboresha maisha yako.
Kwanza kabisa tatizo hili linatokana na nini?
Baadhi yetu huwa tunafikiri tatizo la matumizi mabaya ya fedha yanatokana na fedha. Hivyo tunajikuta tunaipa fedha majina mabaya kama fedha ni mwanaharamu, fedha ni shetani na mengineyo. Tabia zote hizi za matumizi mabaya ya fedha zinaanza na wewe mwenyewe.
Tatizo hili linasababishwa na mambo mengi, hapa nataja baadhi.
1. Ukosefu wa elimu ya matumizi ya fedha. Hili ni tatizo la watu wengi kwa kuwa hakuna sehemu yoyote shuleni ambapo tunafundishwa matumizi ya fedha hasa fedha binafsi. Tabia zetu za matumizi ya fedha tunajifunza kutoka kwa watu wetu wa karibu ambao ni ndugu au wazazi. Hivyo kama wana tabia mbovu kwenye matumizi ya fedha na wewe utakuwa na tabia hizo.
2. Kukosa nidhamu binafsi na nidhamu ya fedha. Ni kwamba huwezi kufanikiwa kwenye jambo lolote kama huna nidhamu binafsi. Kama huwezi kupanga mipango yako na kuifuata basi huna nidhamu kwako mwenyewe na sahau kuhusu mafanikio.
3. Uteja wa starehe. Kuna baadhi ya starehe zina uteja au utegemezi. Vitu kama pombe au madawa ya kulevya vinatengeneza utegemezi mkubwa ambapo mtumiaji analazimika kutumia fedha yoyote anayoipata kukamilisha hitaji lake.
4. Wizi halali. Kuna aina ya wizi mimi huwa nauita wizi halali. Imekaa hivi mtu akijua una hela anakuja kukushawishi uitumie na wewe unaingia kwenye matumizi ambayo wakati mwingine sio muhimu sana kwako. Nimekuwa nikiona mara nyingi mwisho wa mwezi kuna kuwa na matangazo mengi sana ya sehemu za starehe. Hii ni kwa sababu wahusika wanajua mwisho wa mwezi watu wana hela hivyo kuhakikisha wanawashawishi kwenda kuzitumia kwao.
Hizi ni baadhi ya sababu zinazokufanya unakuwa na matumizi mabovu ya fedha na kushindwa kuweka akiba. Kama huzijui sababu hizi ni vigumu sana kuweza kuondokana na tatizo hili.
Unawezaje kutatua tatizo hili?
Moja ya njia za kuondokana na tatizo hili ni kwanza kujua sababu inayosababisha tatizo hili liwepo. Baada ya kujua sababu ndipo sasa utaanza kutatua tatizo kwa kushughulika na sababu hizo.
Pamoja na kujua sababu zinazokufanya wewe ushindwe kuhifadhi fedha kuna mambo mengine muhimu ya kufanya. Mambo hayo ni;
1. Jijengee nidhamu binafsi. Anza kwa kujipa ahadi ndogo na kisha zitekeleze na uendelee kuongeza ahadi hizo. Usikubali tamaa yoyote ikufanye ushindwe kuheshimu mipango yako.
2. Kuwa na bajeti ya matumizi ya fedha kabla hujapata fedha kama ya mshahara. Kwa kuwa umeshaanza kujijengea nidhamu binafsi weka mipango ya matumizi ya fedha zako na uifuate.
3. Angalia aina ya marafiki ulionao au watu unaopendelea kukaa nao. Tabia zako ni wastani wa tabia za watu watano unaopendelea kukaa nao, hivyo kama marafiki zako au watu unaopendelea kukaa nao ni watu wenye matumizi mabaya ya fedha na wewe utakuwa na tabia hiyo. Waangalie vizuri watu unaopendelea kukaa nao na ukiona wana tabia hiyo anza kupunguza muda unaokua nao mpaka kuacha kabisa. Kwa sababu hata ukijijengea nidhamu kama bado utaendelea kuwa karibu na watu hao ni rahisi sana kurudia tabia zako za zamani.
4. Fanya uwekezaji ambao ni vigumu kuchukua fedha zako. Ukiweka fedha benki ni rahisi kuchukua ila kama utaziweka kwenye uwekezaji inakuwa ngumu kidogo kuzichukua. Uwekezaji unaweza kuwa kununua hisa au vipande, kununua viwanja au mali nyingine zisizohamishika kirahisi.