Rais Magufuli aifumua CCM



KAMA falsafa yake inavyojieleza ya ‘Hapa Kazi Tu’, Rais John Magufuli amepeleka falsafa hiyo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kufumua muundo wake baada ya kutangaza kupunguza idadi ya wajumbe wa vikao na idadi ya vikao katika ngazi mbalimbali ili viongozi watumie muda mwingi kufanya kazi za chama.

CCM imesema uamuzi huo, una lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji wa chama na kuongeza muda wa viongozi kufanya kazi za chama kwa umma, badala ya kutumia muda mwingi vikaoni. Sanjari na kufuta baadhi ya vyeo, pia imetangaza uhakiki wa wanachama wake kote nchini na kuanzisha mfumo wa kadi za kielektroniki na kuachana na kadi za sasa, zikiwamo za jumuiya yake ambazo zinafutwa rasmi.

Mabadiliko hayo makubwa ambayo baadhi yanahusisha Kanuni na Miongozo, yataanza mara moja na yale yanayohusisha Katiba ya CCM yatapata idhini ya Mkutano Mkuu utakaoitishwa Februari mwakani, na yamefanywa jana na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) katika kikao chake kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Hicho kilikuwa kikao cha kwanza cha NEC chini ya Mwenyekiti mpya, Rais John Magufuli aliyeteuliwa Julai mwaka huu, akirithi mikoba ya Dk Jakaya Kikwete ambaye jana alimsifu kwa kumuongoza vizuri na kwa hiari yake, kuachia uenyekiti wakati Katiba bado ilikuwa ikimruhusu, akieleza kuwa huo ndio utofauti wa CCM na vyama vingine.

Kwa mujibu wa Katibu wa NEC wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnaye ambaye sasa amepatikana mrithi wake, aliwaeleza waandishi wa habari baada ya kikao hicho kuwa uamuzi huo umefanywa ili kuwa na vikao vyenye tija. Katika fyekafyeka hiyo, wajumbe wa NEC wamepunguzwa kutoka 388 hadi 158, wajumbe wa Kamati Kuu kutoka 34 hadi 24, wajumbe wa Kamati za Siasa za Mikoa wamepunguzwa watatu wakati wilayani wameondolewa wanne pamoja na kufutwa kwa vyeo vya Makatibu Wasaidizi wa Wilaya na Mikoa na wa Mchumi wa Wilaya na Mkoa.

Katika uamuzi huo, imeamuliwa kuwa sasa NEC itakuwa na wajumbe 158 kutoka wajumbe 388 wa sasa, na wajumbe hao wamepunguzwa kutoka miongoni mwao, wakiwamo wabunge ambao sasa watakuwa watano badala ya 10.

#HabariLeo