BARUA YA WAZI KWA MWENYEKITI WA CHADEMA, Freeman Mbowe ,KUTOKA KWA JULIANA SHONZA ,NI MANENO MAZITO AMBAYO LAZIMA YAANGALIWE>>>>

Jina: JULIANA SHONZA

Kabila: Mnyiha wa Mbozi

Elimu: Shahada ya Uzamili (Masters on Sociology) – Shahada ya Uzamivu ( Phd – UDSM) on progress.

Ndoa: Nimeolewa

Umri: Miaka 30

Dini: Mkristo wa Dhehebu la Pentekoste

Kazi: Mbunge wa Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
====================================================


Kama ilivyoelekeza Sheria, na kwa Matakwa ya Kikatiba ninaanza Andiko langu kwa “Kiapo” ili itakapolazimu maneno yangu ya leo yatumike katika mabaraza ya Sheria na Mahakama kama rejea rasmi.

Maana ya neno “kiapo” kama nilivyolitumia linamaanisha kuwa ni maelezo anayotoa mtu ambayo mtu huyo anaamini kuwa ni sahihi na ya kweli. Na kwa kuwa inakubalika katika Sheria (Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6 ya Sheria za Tanzania, kifungu cha 231) kutoa kiapo kwa njia ya maandishi, kama ifuatavyo;

’’Mimi, JULIANA SHONZA, Mtu mzima, Mkristo, Mama wa familia, Mkazi wa Songwe, nikiwa ninaelewa vya kutosha juu ya jambo ninalotaka kulitolea kiapo na hivyo NAAPA kuwa;

NIKIWA NA AKILI TIMAMU BILA KUSHAWISHIWA NA MTU AU KIKUNDI CHA WATU, NAAPA KUWA MAELEZO NITAKAYOYATOA HAPA KUHUSU MHE. FREEMAN AIKAELI MBOWE, (Mb) MWENYEKITI WA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO NI SAHIHI, NA YA KWELI”

Ndugu wana jamvi wenzangu, nikiwa ndani ya kiapo naomba nieleze yafuatayo kuhusu UDHAIFU na UDHALIMU wa NDG. MBOWE, nitajitahidi nielekeze kwa ushahidi wa matukio na kwa ufupi kadri itakavyowezekana.

Nianze kwa kueleza kuwa wengi katika watu wanafahamu (ingawa kuna upotoshaji mkubwa ktk ufahamu huo) kuwa niliondoka / kuondolewa CHADEMA kwa sababu moja tu, nilidiriki kumnyooshea kidole MWENYEKITI MBOWE. Nikikosoa namna ya utendaji wake, nilitia shaka juu ya uwezo, maono, ufundi na maarifa yake katika kumudu aina ya siasa za sasa na hatma ya CHADEMA..nilifanya hivyo kwa maslahi mapana ya CHAMA hicho na NCHI yetu kwa ujumla.

Lakini kama ilivyo kwa viongozi WAOGA (cowards), mkuu wangu huyo (ambae hakuzoea kunyooshewa kidole) aliona nimemtusi, nimemkebehi na nimefanya jambo la kumvua nguo na kumshushia heshima na hakuwa tayari kuvumilia DHIHAKA hiyo..hakuwa tayari kukiri MAKOSA, hakuwa TAYARI kuruhusu UHURU wa kikatiba ulio kwa kila mwanachama wa CHADEMA kutumika, hakuwa tayari kuuona UKWELI, kwa kuwa tu UKWELI huo ulisemwa na JULIANA.

Nitaeleza matukio mawili (kati ya mengi) ambayo nilimkosoa MBOWE na ikawa mwanzo wa mtafaruku baina yetu na baina yangu na CHADEMA.

(a) Mnamo tarehe 16 Mei, 2012; (Kwa maelekezo ya MBOWE) Aliyekuwa Mwenyekiti wa BAVICHA Mhe John Heche alitoa tamko la kumtuhumu Ndg John Magale Shibuda kuwa ni MSALITI kwa kitendo chake cha kutangaza hadharani kuwa atagombea URAIS kupitia CHADEMA mwaka 2015.


Baada ya TAMKO hilo, (nikiwa Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA) nilijitokeza hadharani kumpinga HECHE, na kumkosoa kuwa TAMKO lake halina Baraka za BAVICHA kwani hajamshirikisha Kiongozi yeyote wa BAVICHA na halikupitia vikao rasmi vya kikatiba, hivyo nikasema kuwa TAMKO hilo ni la HECHE na wala sio la BAVICHA, na nikasema kuwa hatuko tayari BAVICHA kutumika na MTU ndani ya Chama kupambana na MTU mwingine.


Mnamo tarehe 26/5/2012, Mnadhimu na Mjumbe wa Kamati Kuu wa CHADEMA Mhe Tundu Lissu (kwa maelekezo ya Mbowe) akajitokeza hadharani na kusema HECHE yuko sahihi, na kwamba SHIBUDA ni pandikizi na msaliti. Kwa mara nyingine nikapinga hoja ya Lissu iliyonukuliwa kwenye Gazeti la Mwananchi la tarehe 27/5/2012 ukurasa wa 7. Nilisema Mwenyekiti HANA Absolute Mandate ya kuitumia BAVICHA anavyopenda.


(b) Mnamo tarehe 2, february 2013 katika vuguvugu la Mhe Zitto Kabwe kutangaza kuwania UENYEKITI wa CHADEMA na mimi kuhisiwa kuwa ni miongoni mwa wanaomuunga mkono, niliitwa na kutakiwa kujieleza hasa kutokana na hekaya iliyoitwa Ripoti ya Siri ya Mwenendo wa Kisiasa wa Zitto Z. Kabwe ndani na nje ya CHADEMA. 


Kwa kuwa niliamini katika kweli, sikushindwa kutamka mbele ya kikao kile ambacho Mhe Baregu alikuwepo, Mbowe mwenyewe alikuwepo na Dr Kitila (akiwa bado CHADEMA) alikuwepo kuwa sina IMANI na uwezo na maarifa ya Mwenyekiti kukivusha Chama katika wakati huu, ni vyema na ni kutokana na utaratibu wa kidemokrasia ndani ya Chama uliokuwepo kikatiba watu wengine waruhusiwe kugombea na ikiwa wanachama wengi watakubali kufanya mabadiliko ya Mwenyekiti, UAMUZI wao uheshimiwe, miongoni mwa wanaotaka mabadiliko hayo ni pamoja na Mimi.

Baada ya Mjadala mrefu, nilijiengua/kuenguliwa CHADEMA kwa jina maarufu la wakati huo la MSALITI, maana kila aliyempinga MBOWE wakati huo na hata sasa aliitwa hivyo.

Baada ya kueleza kwa ufupi matukio hayo mawili yaliyothibitisha udhalimu wa Mbowe wa kutumia mabavu kuendesha Chama na kufanya maamuzi na kuonyesha alivyo Kiongozi Dhaifu, mwenye Woga na asiyejiamini (maana siku zote amekuwa akituma watu badala ya kujitokeza yeye mwenyewe), nirudi katika kadhia ya maamuzi ya Kamati Kuu ya CHADEMA iliyokutana Juzi na kuunda UKUTA.

Kwanza ieleweke kuwa sio mara ya kwanza CHADEMA kuunda opresheni zisizo na mbele wala nyuma, ila mwaka huu operesheni hii imezidi kuwa ya hovyo kuwahi kufanywa ndani ya CHADEMA..eti ya kuzuia UDIKTETA..Hivi baada ya yoooote aliyoyafanya MBOWE ndani ya CHADEMA anapata wapi authority, ama legitimacy ya kukemea Udikteta..?

Mimi najua kuwa CHADEMA ya sasa sio ile niliyokuwa mimi miongoni mwa Viongozi, maana sisi tulikuwa tunahoji na wakati mwingine kupinga UJINGA na UONEVU ndani ya Chama, hii ni CHADEMA ya ma-ZOMBIE yanayofuata kama WAFU wasio na roho wala maono. Chadema yenye Katibu Mkuu aliyefungwa hatamu, akivutwa kulia anakwenda na akivutwa kushoto ndio unakuwa muelekeo wake, yenye Viongozi wa BAVICHA waoga, wajinga, wasiofikiri, wasiojiuliza, wenye njaa na wanaojali maslahi ya matumbo yao na matumbo ya waliowaweka madarakani.

Ili nifanye thread hii kuwa fupi naomba nifanye marejeo ya Thread yangu ya tarehe 24 february, 2016 yenye anuaniUshauri kwa Jirani: Mbowe must be disposed! na nyingine ni hii Waraka kwa vijana wa UKAWA: Ni wakati wa Mabadilikohizo nyuzi mbili zinawatosha kabisa kuwa ni hadidu za rejea juu ya mwenendo na tabia zinazoonyesha udhaifu mkubwa wa MBOWE na matendo yake.

Kimsingi, operesheni hii nayo itakufa kifo cha kimya kimya kama ilivyo zingine zilizowahi kutangazwa huko nyuma bila kuacha mafanikio ya aina yeyote, ila kitu cha kipekee sana ambacho nikiri kuwa huko nyuma hakikuwahi kujitokeza ni jina lenyewe la operesheni, inaitwa Operesheni UKUTA...woow, what a brand name..!!!