Afikishwa Mahakamani kwa Kumuita Rais Magufuli ni Kilaza
ELIZABETH Asenga (40), mkazi wa jijini Dar es Salaam amepandishwa kortini jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kuandika maneno ya kumkashifu Rais John Magufuli kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp.
Akisomewa mashtaka yake na Leonard Chalu, wakili wa serikali, mbele ya Hakimu Huruma Shahidi, mwanamama huyo, alidaiwa kufanya kitendo hicho kilicho kinyume na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.
Wakili Chalu alidai kuwa, mnamo tarehe 06 Agosti mwaka huu, mtuhumiwa huyo aliandika kwenye mtandao wa what’s App ujumbe uliosomeka;
“….Rais kilaza kama huyu wetu, angalia anampa Lissu umashaghuli… f****l** lile, kwanza picha yake ukiweka ofisini ni nuksi tupu na ukiamka asubuhi ukakutana na picha yake, siku yako inakuwa ina mkosi mwanzo mwisho.”
Hata hivyo, mshitakiwa Elizabeth, alikana mashtaka hayo huku wakili wa serikali akidai kuwa, upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.
Mtuhumiwa alipewa dhamana yenye masharti yanayohitaji wadhamini wawili huku kila mmoja akitakiwa kusaini hati ya shilingi 3 millioni.
Kesi hiyo imeahirishwa na inatarajia kutajwa tena mnamo tarehe 22 Septemba, mwaka huu.
CREDIT: TANZANIA DAIMA