Rais wa Ufilipino ajutia matamshi yake kwa Obama
Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte ameelezea kusikitishwa na matamshi yake yaliyohusisha lugha chafu na kutoa taswira ya kumshambulia rais Barack Obama wa Marekani.
Katika taarifa yake ameeleza kwamba lengo lao la msingi ni kuweka sera ya kimataifa ya kujitegemea wakati wakihamasisha uhusiano wa karibu na mataifa yote hasa Marekani ambayo imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu.
Kabla ya kuondoka Jumatatu kuelekea katika mkutano wa kikanda huko Laos, Duterte alimuonya rais Obama kutomfundisha namna ya kupambana na wasafirishaji wa dawa za kulevya.
Mapambano hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,000 toka alipoingia madarakani mwezi Juni.
Kufuatia kauli za rais huyo wa Ufilipino, rais Barack Obama alifuta mkutano wake uliokuwa umepangwa na badala yake atakuwa na mkutano na kiongozi wa Korea Kusini.