Mbowe amtaka JPM amtumbue Waziri Mkuu Kassim Majaliwa .

Baada ya swali lake kwa Waziri mkuu kuhusu tuhuma za rushwa kwa wabunge wa CCM kuzuiliwa na Naibu Spika kwa kile kilichoelezwa kuwa nje ya utaratibu, Kiongozi aa kambi ya upinzani Bungeni, Freeman Mbowe jana aliitisha mkutano na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Bunge mjini Dodoma, akiwa na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu na viongozi wengine wa Chama cha Wananchi (CUF). Katika mkutano huo, Mbowe alimtaka Rais Magufuli kumtumbua Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kile alichoeleza kuwa yeye (Majaliwa) pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana walihusika kutoa kwa wabunge hao wa CCM 272 fedha hizo.

Alisema pia kuwa, wanamuandikia barua Rais kutaka aunde Tume ya Kimahakama ya Uchunguzi, kuchunguza suala hilo kwa kuwa linawahusu wabunge, na Bunge haliwezi kujichunguza lenyewe.

Akifafanua kuhusu fedha hizo, Mbowe alisema taarifa walizonazo, zinathibitisha kuwa katika kikao cha wabunge wa CCM cha Oktoba 25, mwaka huu, Majaliwa na Kinana waligawa fedha Sh milioni 10 kwa kila mbunge wa CCM ili kuwapooza kuhusu hali ya mdororo wa uchumi.

Alisema pia kuwa fedha hizo, zilizoanza kutolewa Oktoba 26, zililenga pia kuwashawishi wabunge hao wa CCM, kupitisha Muswada wa Huduma za Habari wa mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/18, ambao mapendekezo yake yamewasilishwa bungeni.

Mbowe alisema tuhuma hizo ni nzito na Bunge haliwezi kujichunguza lenyewe, hivyo ni lazima iundwe tume huru ya kimahakama kuchunguza jambo hilo. Mbowe alisema ushahidi wa kutosha wanao na watautoa mbele ya tume hiyo.

Mbowe alisema walimshangaa Naibu Spika, Dk Akson kwa kuwazuia kutoa ushahidi ndani ya Bunge, kama walivyoombewa mwongozo na Nkamia. Alieleza kuwa hiyo ni mara ya kwanza kwa upinzani, kuzuiwa kutoa ushahidi kwa jambo, ambapo linaonekana kama ni uongo.

Lissu naye azungumza

Kwa upande wake, Lissu alisema watamuandikia Rais Magufuli barua rasmi kueleza kilichofanywa na viongozi wake, na kumtaka achukue hatua kuhusu suala hilo. #HabariLeo