ZIJUE FAIDA ZA PAPAI KATIKA TIBA
Mimea na matunda imekuwa ikitumika na wazee wetu kama dawa, hii ni kwa sababu vizazi vilivyopita kwa maana ya babu na bibi zetu hawakuwahi kuwa na hospitali wala zahanati kwa ajili ya kupata tiba, isipokuwa walikuwa wakitumia mimea kwa ajili ya chakula na tiba.
Kuna mimea mbalimbali pamoja na matunda ambayo tumezoea kuitumia bila hata kujua umuhimu wake kiafya. Ni dhahiri kuwa baadhi ya mimea huweza kutumika kama tiba katika miili yetu, tena tiba salama kabisa zisizo hata na chembe ya kemikali ambazo huwa na madhara kwa afya zetu.
Kutokana na suala hili leo kuptia tovuti hii tutakwenda kufahamu namna mmea wa mpapai unavyoweza kuwa tiba nzuri kwako ikiwa ni kuanzia kuanzia mizizi, shina, majani na hata matunda yake pia.
Asili ya mpapai ni Amerika ya kati, ambapo kuanzia matunda, majani na utomvu wa mmea huu huweza kutumiwa kama dawa maeneo mbalimbali duniani. Vile vile, matunda na utomvu wake yamekuwa yakitumika kutengeneza pombe na mvinyo katika baadhi ya nchi, huku wengine wakitumia mpapai kama dawa kwa mifugo na binadamu.
Inaelezwa kuwapo na utafiti zilizowahi kufanyika na kuchapishwa katika jarida lijulikanalo kwa jina la ‘Archieve’ la nchini India mnamo Oktoba 27 mwaka 2010, ambapo jarida hilo lilieleza kwamba juisi ya majani ya mpapai iliweza kusaidia wagonjwa watano waliowahi kupata homa ya dengue.
Mbali na utafiti huo, pia kuna tafiti zilizowahi kufanywa na madaktari wa nchini Marekani na Japani na kubaini kuwa, juisi ya majani ya mpapai ina uwezo wa kutibu malaria na saratani, japokuwa tafiti hizo hazikukubawaliwa kisayansi.
Aidha, wataalam wa lishe nao wanaeleza kwamba, watu wenye matatizo ya kupatwa na majipu, uvimbe na vidonda mara kwa mara huwa na upungufu wa virutubisho muhimu, ambavyo huweza kupatikana ndani ya papai, hivyo imegundulika watu wenye matatizo hayo wakitumia papai hupata nafuu na kupona haraka.
Pia papai husaidia kuleta nuru ya macho, kama inavyoaminika kwa karoti, hali kadhalika papai pia husaidia kupunguza madhara yatokanayo na moshi wa sigara.
Hivyo wavutaji wa sigara ni vyema wakatumia tunda hili mara kwa mara ili kujipunguzia madhara ya moshi wa sigara, ingawaje ni vyema wakakumbuka matumizi ya sigara si mazuri kwa afya hivyo ikibidi ni vizuri kuacha kabisa.
Ni wazi kuwa papai ni tunda lililosheheni kila aina ya utajiri wa vitamin kuliko matunda mengine, kwani lina vitamin A, B, C, D na E.
Wataalam wa tiba za asilia pia wanaeleza kwamba tunda hili linauwezo wa kutibu tatizo la usagaji wa chakula tumboni pia hutibu kisukari na pumu na mara nyingine hata kifua kikuu.
Sambamba na hayo, wataalam pia wanaeleza kwamba utomvu wa mmea wa mpapai hutibu magonjwa ya ngozi kama vile ukurutu, mapunye na hata majeraha ya moto, kiungulia na vidonda pia.
Mbali na hayo, imeelezwa kuwa mbegu za tunda la papai hutibu ini, huku majani yake yakisaidia kutibu shinikizo la damu na hata mbegu zake pia hutibu homa.
Hali kadhalika mizizi ya mmea wa mpapai husaidia kuzuia kutapika, lakini pia papai linaweza kutumika kama kilainisho cha nyama ili iweze kuiva vizuri, hususani nyama ya ng’ombe.
Kwa kutambua baadhi ya faida hizo za mpapai sasa ni vizuri ukaanza kutumia rasilimali hii ya mimea na matunda tuliyotunukiwa na Mola wetu, ili kujiepusha na madhara yatokanayo na maradhi mbalimbali.