BILIONI 2.7 ZAPOTEA MRADI WA HOSPITALI MONDULI,WAZIRI MKUU AAGIZA UCHUNGUZI UFANYIKE
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo kufanya uchunguzi na kumpelekea taarifa ya watendaji waliohusika katika ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa mradi wa hospitali ya wilaya ya Monduli uliogharimu sh. bilioni 2.7.
Ametoa agizo hilo jana (Jumapili, Desemba 4, 2016) wakati akizindua hospitali ya wilaya ya Monduli ambayo katika ujenzi wake kulitakiwa kuwe na jengo la maabara ambalo halipo na fedha zimeisha.
"Mkuu wa Mkoa shirikiana na Sekretarieti yako kufanya uchunguzi na atakayebainika kuhusika kwenye ubadhirifu huu achukuliwe hatua za kisheria kwa sababu ujenzi huu ulihusisha na jengo la maabara lakini tayari mradi umekamilika na hakuna jengo la maabara," alisema.
Naye Mkuu wa mkoa huo Bw. Gambo alisema tayari wameanza kufanya uchunguzi wa ujenzi wa mradi huo baada ya kubaini kuwa umetumia kiasi cha fedha kilichotumika hakilingani na thamani ya mradi huo.
Mkuu huyo wa Mkoa aliahidi kufuatilia suala hilo na uchunguzi utakapokamilika taarifa hiyo itapelekwa kwa Waziri Mkuu.
Awali, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Zaveri Benela akisoma taarifa ya hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto ya jengo la upasuaji karibu na wodi ya wazazi hali inayowalazimu kuwasafirisha wagonjwa umbali wa zaidi ya mita 300 hadi kwenye jengo la upasuaji lililopo katika majengo ya zamani.
Pia kukosekana kwa jengo la wagonjwa wa nje na jengo la maabara kwenye majengo hayo mapya hali inayochangia huduma kutolewa kwenye maeneo miwili tofauti kwa wakati mmoja yaani katika wodi mpya na majengo ya zamani na hali hivyo inaleta usumbufu kwa wagonjwa.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ametoa siku saba kwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Bw. Idd Kimanta kumaliza tatizo la mgogoro wa ardhi katika kijiji cha Emairete kilichopo Monduli juu mkoni hapa baada ya kudumu kwa miaka 20.
Mgogoro huo ni wa shamba kubwa ambalo awali lilikuwa linamilikiwa na kampuni ya bia ya Breweries na kisha kurejeshwa kwa kijiji hicho ambapo viongozi wa zamani wa Kijiji hicho walijimilikisha kinyemela.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya kusimamishwa na wanakijiji hao waliokuwa wamebeba mabango ya kumuomba msaada wa kutatuliwa kwa mgogoro huo wakati anatoka kudhuru kaburi la Waziri Mkuu wa zamani Hayati Moringe Sokoine.
Waziri Mkuu alimtaka mkuu huyo wa wilaya kueleza sababu za kwa ya nini uongozi wa wilaya umeshindwa kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ambaye alifika kijijini hapo na kutoa maelekezo.
Baada ya maelekezo hayo Waziri Mkuu aliwataka wananchi hao kuendelea kuwa na imani ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli ambayo ipo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi hasa wanyonge.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo alikiri kuwepo kwa mgogoro huo kwa miaka 20 na kwamba Waziri Lukuvi alitoa maelekezo ambayo halmshauri inayafanyia kazi na imeshindwa kuleta majibu kwa wananchi hao kutokana na ziara ya Waziri Mkuu ambaye aliwataka watekeleze majukumu yao na wasitumie ziara yake kama kisingizio.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alisema Serikali na Watanzania wote wanatambua na kuiheshimu kazi nzuri iliyofanywa na hayati Sokoine kwa Taifa kipindi cha uhai wake na itaendelea kuienzi. Pia Serikali itaendelea kushirikiana na familia katika mambo mbalimbali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU