Rage Atema cheche asema Yanga inyang’anywe pointi zote kwa kumtumia Kessy
Rage ameitaka klabu ya Simba kutokubali kudhalilishwa kwa kukubali milioni 50 badala yake wadai bilioni 1.2 na Yanga ipokwe pointi zote
Mwenyekiti wa zamani wa Simba Ismail Rage ameitaka klabu ya Simba kwenda mbele zaidi kudai haki yao na si kukubali kiasi cha shilingi milioni 50 kama fidia kama livyoamriwa na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji.
Katika hatua nyingine Rage amesema, Yanga inatakiwa kupoteza pointi zote katika michezo ambayo walimtumia Hassan Ramadhani Kessy kwenye kikosi chao.
“Maadam TFF wanakiri kwamba Kessy alikuwa mchezaji halali wa Simba SC na Yanga wamevunja mkataba kabla ya wakati, Yanga wanatakiwa wanyang’anywe pointi zote walizoshinda dhidi ya timu nyingine kabla ya uamuzi wa TFF,” amesema Rage wakati akihojiwa na kipindi cha michezo cha Sports Extra cha Clouds FM .
“Simba wanatakiwa wasichukue hizo milioni 50 watakuwa wamejidhalilisha sana, kwa mujibu wa mkataba wa Simba, wanatakiwa wapate 1.2 billion kama dola za 600,000 kimarekani. Waende FIFA kwa ushahidi wote uliokuwepo na TFF wameshiriki kuvunja mkataba kwahiyo ushahidi upo wa kuwatia hatiani Yanga.”
“Kessy alikwenda Uturuki na Yanga wakati bado anamkataba na Simba, akaenda Algeria wakati bado yupo ndani ya mkataba, wakienda ubalozi watakuta ushahidi lakini wakienda uhamiaji watapata pia ushahidi.”