Alichokizungumza Mwanasheria wa ChademaTundu Lissu kuhusu mbunge wa kilombero kufungwa miezi 6

HATUA ya Mahakama ya Wilaya ya Kilombero, Morogoro kumfunga Peter Lijualikali, Mbunge wa Jimbo la Kilombero miezi sita jela, inatokana na visa vya kisiasa.
Ni kauli ya Tundu Lissu, Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo mbele ya waandishi wa habari aliokutana nao kwenye Makao Makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki amesema kuwa, vita kati ya upinzani na Chama Cha Mapinduzi (CCM) vimesababisha Lijuakali (Chadema) kupata hukumu hiyo ya kisiasa.


Mbele ya waandishi wa habari Lissu amesema kuwa, “hiyo ni hukumu ya kisiasa” na kwamba, Jeshi la Polisi nalo limeingizwa kwenye vita hivyo.

Lissu amesema, chanzo cha hukumu hiyo kinatokana na mgogoro wa uongozi ndani ya Halmashauri ya Kiliombero ambapo Chadema na washirika wake wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walishinda madiwani wengi.

Hivyo, kwa mujibu wa Lissu, Halmashauri ya Kilombero ilipaswa kuongozwa na mwenyekiti anayetoka na Ukawa na awe Chadema.

“Ili hilo lisiwezekane, na ili CCM wachukue Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero licha ya kushidwa kwenye udiwani, ilibidi wamfanyie Lijualikali mambo ya ajabu,” amesema Lissu.

Lijualikali (30) amehukumiwa jana kwa kosa la kufanya fujo na kusababisha taharuki. Huku Stephano Mgata (35), Dereva wake ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo akifungwa kifungo cha miezi sita nje.

“Kifungo cha Mh. Lijualikali ni adhabu ya kisiasa. Mh Lijualikali ni mfugwa wa kisiasa. Amefugwa kwa sababu ya siasa.

“Adhabu ya kisisa ni vita ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi ya Chadema na wanatumia Jeshi la Polisi, wanatumia mahakama na kwingineko. Vita hii hii wanawatumia akina Lipumba (Profesa Ibrahim Lipumba,” amesema Lissu na kuongeza;


“Kwingine wamemweka Lema (Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini) mahabusu kwa miezi mitatu. Hakuna jinai yoyote. Tuliwashinda kwenye uchaguzi.

“Sasa baada ya uchaguzi walimfungulia Lijualikali kesi ya kupinga matokeo mahakama kuu, tukawapiga chini. Wamefungua rufaa na tunawatandika.”

Mwanasheria huyo amesema kuwa, nchi hii ina wafungwa wa kisiasa na kwamba, pamoja na CCM kudhani kwamba, kumfungulia kesi Lijuakali kutawapa afueni. Wasahau.

“Tuna wafungwa wa kisiasa nchi hii. Wale wanaofikiria kwamba kumfunga Lijualikali CCM itapendwa na wananchi wa kilombelo wasahau hilo.
“Huwezi kuwatesa wananchi, ukatesa viongozi waliowachagua kwa mapenzi yao halafu ukategemea wakupende. Wasahau,” amesema Lissu.


Aidha, Lissu ametoa ufafanuzi kuwa Ibara ya 67 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamlinda Lijualikali hivyo hawezi kupoteza ubunge wake kutokana na hukumu hiyo.

Amesema Chadema hakijaridhika na hukumu hiyo, hivyo kwa sasa wanaandaa utaratibu wa kisheria ili kukata rufaa kuipinga ambapo hatua hiyo inaweza kuchukua siku mbili kukamilika.

Timothy Lyon, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo alisema, amemhukumu Lijualikali baada ya kumtia hatiani kwa kosa yeye na dereva wake na kwa kuwa, mbunge huyo alipatikana na hatia katika kesi tatu huko nyuma na kuhukumiwa kulipa faini hivyo alistahili kutumikia adhabu hiyo.

Kesi zilkizotajwa na Lyon zinazomuhusu Lijualikali ni namba 338, namba 220 na namba 340 zote za mwaka 2014.

Katika kesi hiyo, Dotto Ngimbwa, Inspekta wa Polisi aliiambia mahakama kuwa, Lijuakali akiwa mshtakiwa namba moja pamoja na Mgata walitenda kosa hilo Machi Mosi mwaka 2016 eneo la Kibaoni katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kialombero na kwamba, walifanya fujo kinyume cha sheria.

Alisema tukio hilo lilitokea Machi Mosi mwaka huo saa 4 asubuhi ambapo washtakiwa walikana mashtaka lakini upande wa mashtaka ukathibitisha bila kuacha shaka kwamba, walitenda kosa.