Anne Kilango Malecela aongeza joto mabadiliko ya mawaziri


MBUNGE mteule Anne Kilango Malecela amesema ameupokea uteuzi wa ubunge wa Rais John Magufuli juzi, na kusema kuwa Mungu ana sababu za kumrejesha tena katika nafasi hiyo, ambayo ameifanyia kazi kwa muda wa miaka 15.

Uteuzi wa Kilango unazidi kuongeza joto kuwa huenda kukafanyika mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, ukizingatia uteuzi uliofanywa na Dk Magufuli wiki iliyopita wa kumteua aliyekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu), Dk Abdallah Possi kuwa Balozi; pamoja na uteuzi wa wabunge wengine wawili.
Kabla ya Anne Kilango, Dk Magufuli pia alifanya uteuzi wa wabunge wengine wawili, Profesa Palamagamba Kabudi na Abdallah Bulembo kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika nafasi zake 10 alizonazo kwa mujibu wa Katiba.

Juzi usiku, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilitangaza kuwa Rais Magufuli amemteua Anne Kilango Malecela kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwamba ataapishwa kwa mujibu wa taratibu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kilango alisema anamshukuru Mungu pamoja na Rais Magufuli kwa kuwa na imani naye na kuamua kumteua tena katika nafasi hiyo. “Kwa kweli sina maneno mengi, namshukuru Mungu na pia ninamshukuru Rais wangu kwa kuwa na imani tena kwangu na kuamua kunipa nafasi hii. Nimekuwa mbunge kwa miaka 15, ni kazi ninayoielewa na ninamuomba Mwenyezi Mungu aniwezeshe ili nifanye kazi itakayowaridhisha,” alisema mbunge huyo wa zamani wa Same Mashariki mkoani Kilimanjaro, ambako alihudumu kwa miaka 15 hadi aliposhindwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Mbunge huyo mteule alisema pia anakwenda bungeni kwa ajili ya serikali, wananchi pamoja na kwenda kukitetea chama chake (Chama Cha Mapinduzi) pamoja na kurekebisha pale panapostahili, lengo likiwa ni kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk Magufuli. #PeruziNaKudadisi #HabariLeo