BARAZA la Mitihani la Taifa (Necta) :Kidato cha kwanza kupimwa na Necta kwa mitihani maalum.
BARAZA la Mitihani la Taifa (Necta), linatarajia kuanza upimaji maalumu wa stadi na maarifa kwa wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu shule za Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana jana kutoka Necta na kusainiwa na Kaimu Mtendaji, Dk. Richard Kasuga, makatibu tawala Tanzania Bara wanajulishwa kuanza kufanikisha mchakato huo na upimaji huo unatarajiwa kuanza Februari 28, mwaka huu.
Ilifafanua kuwa wanafunzi wote waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu wanatakiwa kufanyiwa mtihani maalumu kwa ajili ya kuwapima ili kubaini uwezo wao waliouonesha katika mitihani yao ya shule ya msingi.
Iliongeza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuwabaini wanafunzi waliofaulu kwa njia ya udanganyifu na watakaobainika wataondolewa shuleni.