YANGA YAFANYA MAUAJI COMORO, YATOA KIPIGO KIZITO DHIDI YA NGAYA DE MBE YA COMORO


Yanga imeanza kwa kasi michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwafunga wenyeji wao Ngaya de Mbe ya Comoro mabao 5-1


Kikosi cha Yanga kimeanza kwa kasi michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwafunga wenyeji wao Ngaya de Mbe ya Comoro mabao 5-1.

Kipigo hicho kinaifanya Yanga kuwa na kazi nyepesi katika mchezo wa marudiano ambao utapigwa uwanja wa Taifa Dar es Salaam Jumamosi ijayo.Wawakilishi hao wa Tanzania katika michuano hiyo mi kubwa Afrika walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao mawili yaliyofungwa na kiungo Mzambia Justine Zullu na winga Simon Msuva.

Zullu akilifunga bao lake la kwanza tangu atue Yanga dakika ya 43, akimalizia kazi nzuri ya Simon Msuva na wakati mashabiki wa Ngaya de Mbe wakiamini watakwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao moja Msuva alifunga bao la pili dakika ya 45 kazi nzuri ya Haruna Niyonzima.

Yanga ilirudi kwa kasi kipindi cha pili na iliwachukua dakika 9 kufunga bao la pili mfungaji akiwa Mzambia Obrey Chirwa ambaye alimalizia kazi nzuri ya Msuva.

Dakika ya 65 Amissi Tambwe aliifungia Yanga bao la nne baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Niyonzima na kuwakatisha tamaa wenyeji wao Ngaya.

Ngaya walionekana kuzidi kupambana wakitafuta angalau bao la kufutia machozi na jitihada zao zilizaa matunda dakika ya 66 baada ya Said Anfane kufunga bao zuri akimalizia krosi iliyochongwa kutoka winga ya kushoto mwa lango la Yanga.

Baada ya kufungwa bao hilo Yanga walikuwa juu na kuanza kulisakama lango la Ngaya ambapo dakika ya 73 Thabani Kamusoko alifunga bao la pili baada ya kupokea pasi nzuri ya Juma Mahadhi aliyeingia muda fupi kuchukua nafasi ya Tambwe.

Mchezo huo uliendelea kwa timu zote kushambuliana hasa Yanga ambao alipoteza nafasi mbili za wazi katika dakika za 78 na 80 ambapo Mahadhi alishindwa kutumia na kuzitumia nafasi hizo.

Hadi filimbi ya mwisho Yanga iliibuka na ushindi huo mnono ambao sasa itahitaji nguvu kidogo katika mchezo wa marudiano ili kusonga mbele raundi ya kwanza ya michuano hiyo.