YANGA YATOA KIPIGO KIZITO DHIDI YA KAGERA SUGAR UWANJA WA KAITABA, HISTORIA MPYA YAANDIKWA



Story kubwa katika anga la michezo hapa Bongo ni namna ambavyo mchakato wa mabadiliko ya klabu ya Yanga unavyozidi kuchua sura mpya kila kukicha, lakini ukiweka hilo kando, October 22 Yanga imetoa dozi ya maana kwa Kagera Sugar kwa kuichakaza bao 6-2 katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara.

Kagera Sugar ikiwa kwenye uwanja waje wa nyumbani Kaitaba, imeshindwa kuzuia mvua ya magoli kutoka kwa watoto wa Jangwani na kujikuta wakilazimishwa kuwa timu ya kwanza kuchezea kichapo kikubwa msimu huu huku Yanga ikiwa timu ya kwanza kufunga magoli mengi kwenye mechi moja hadi sasa tangu kuanza kwa msimu.

Kagera Sugar ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza kupitia kwa Mbaraka Yusuf katika dakika ya tatu kipindi cha kwanza akiachia shuti kali lililombabatiza Vicent Andrew na kutinga wavuni lakini Donald Ngoma akaisawazishia Yanga dakika mbili baadaye kwa kuunganisha kwa kichwa pasi kutoka kwa Simon Msuva.

Simon Msuva akafunga bao la pili baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na golikipa wa Kagera Sugar Hussein Sharif ‘Casillas’ wakati akiokoa shuti kali la Haruna Niyonzima.

Yanga wakapata goli la tatu lililofungwa na Obrey Chirwa baada ya Casillas kutema mpira kwa mara ya pili na kutoa mwanya kwa Chirwa kufunga goli rahisi katika mchezo huo.

Dakika tatu baada ya timu kutoka mapumziko, Mbaraka Yusuf mfungaji wa bao la kwanza la Kagera Sugar akaifungia timu yake bao la pili na kufanya matokeo kusomeka Kagera Sugar 2-3 Yanga.

Mvua ya magoli ilizidi kuendelea kuiandama Kagera Sugar baada ya Deus Kaseke kupachika bao la nne kwa kuunganisha krosi ya Simon Msuva. Chirwa akafunga bao lake la pili katika mchezo huo huku likiwa ni bao la nne tangu ajiunge na klabu hiyo akitokea FC Platinum ya Zimbabwe.

Donald Ngoma akakamilisha ushindi wa pili wa Yanga katika Kanda ya Ziwa kwa kufunga bao la 6.

Rekodi
Msimu uliopita October 31, 2015 Simba iliifunga Majimaji FC bao 6-1 kwenye uwanja wa taifa ambacho kilikuwa kipigo kikubwa zaidi katika msimu huo.
Yanga imekuwa klabu ya kwanza msimu huu kufunga magoli mengi (6) katika mechi moja huku Kagera Sugar wao wakiweka rekodi ya kufungwa magoli mengi (6) katika mechi moja tangu kuanza kwa ligi msimu huu 2016-17.
Magolikipa wawili wamecheza mechi moja na kufungwa idadi sawa ya magoli katika vipindi tofauti vya mchezo mmoja. Kagera ilimuanzisha Hussein Sharif katika kipindi cha kwanza akaruhusu magoli matatu akatolewa nafasi yake ikachukuliwa na David Burhan ambaye nae akafungwa magoli matatu.
Donald Ngoma na Obrey Chirwa wachezaji wa zamani wa FC Platinum wamefunga magoli mawili kila mmoja kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar.
Chirwa amefanikiwa mufunga magoli manne baada ya kucheza nne za hivi karibuni. Goli lake la kwanza Yanga na VPL lilikuwa dhidi ya Mtibwa Sugar, mechi dhidi ya Azam hakufunga, akafunga goli lake la pili dhidi ya Toto African kabla ya kufunga mawili dhidi ya Kagera Sugar.
Magoli manne ya Chirwa yanamfanya amfikie mshambuliaji mwenzake wa timu hiyo mrundi Amis Tambwe.
Magoli nane yamefungwa katika mechi moja (magoli mengi zaidi kufungwa katika mechi moja hadi sasa) kwenye ligi.