SIMBA YAFUTA UTEJA KWA TOTO AFRICANS BAADA YA KUIPA KIPIGO KIZITO UWANJA WA UHURU



Hatimaye Simba imefuta uteja kwa Toto Africans baada ya kuifunga bao 3-0 kwenye uwanja wa Uhuru.

Kabla ya mchezo wa leo, Simba ilikuwa haijawahi kutoka na pointi zote tatu katika mechi sita zilizopita. Kama unakumbukumbu nzuri, msimu uliopita Simba ililazimishwa sare ya goli 1-1 kwenye mchezo wa raundi ya kwanza CCM Kirumba lakini ikafungwa 1-0 kwenye mchezo wa marudiano uwanja wa taifa.

shindi wa leo (October 23, 2016), ni ushindi wa nne mfululizo kwa Simba huku ukiwa ni ushindi wao wa tisa katika mechi 11 walizocheza msimu huu.

Rekodi ya kutofungwa bado inaendelezwa na vijana wa Msimbazi chini ya kocha wao Joseph Omog wakiwa tayari wamecheza mechi 11 wakifanikiwa kushinda michezo tisa na sare mbili.

Mchezo wa leo

Magoli ya Simba yamefungwa na Muzamiru Yassin ambaye alianza kufunga goli la kwanza dakika ya 43 baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Fredick Blagnon.

Laudit Mavugo aliyeingia kutoka benchi kuchukua nafasi ya Blagnon aliifungia Simba bao la pili dakika ya 52 akitumia vyema pasi ya Ibrahim Mohammed.

Bao la tatu la Simba lilifungwa na Muzamiru Yassin dakika ya 74 na kuhitimisha ushindi uliokuwa ukisubiriwa na mashabiki wa Simba baada ya timu yao kucheza mechi nyingi bila ushindi mbele ya Toto Africans.

Ndondoo
Simba ilikuwa hajashinda mechi 6 za mwisho dhidi ya Toto Africans kabla ya mchezo wa leo. Mechi 6 ni sawa na misimu mitatu.
Mechi 6 za mwisho ambazo Simba wamekutana na Toto bila kupata ushindi ni pamoja na 21/09/11 Toto Africans 3-3 Simba, 11/03/12 Simba 0-0 Toto Africans, 10/11/12 Simba 0-1 Toto Africans, 30/03/13 Toto Africans 2-2 Simba, 19/12/15 Toto Africans 1-1 Simba, 17/04/16 Simba 0-1 Toto Africans, (mchezo wa leo 23/10/16 Simba 3-0 Toto Africans).
Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 29 baada ya kucheza mechi 11 za ligi kuu Tanzania bara.
Toto Africans inaburuza mkia kwenye msimamo wa ligi, imefanikiwa kupata pointi 8 katika mechi 12 ambazo imecheza hadi sasa.
Simba imeshinda mfululizo mechi zake 4 za mwisho kwenye ligi na kufanikiwa kufunga magoli 8 bila kuruhusu goli. Toto Africans imepoteza mechi zake zote nne za mwisho huku ikiwa imebugizwa magoli 10 wakati yenyewe imefunga magoli mawili katika mechi nne zilizopita.
Mzamiru Yassin amefunga magoli manne katika mechi tatu mfululizo za mwisho za Simba. Alifunga bao lake la kwanza dhidi ya Kagera Sugar (Simba 2-0 Kagera Sugar), akafunga goli pekee dhidi ya Mbao FC (Simba 1-0 Mbao FC) kabla ya leo kufunga magoli mawili dhidi ya Toto Africans (Simba 3-0 Toto Africans).