Hotuba ya Waziri Mkuu ya kuahirisha mkutano wa tano wa Bunge la 11 Novemba 11 2016
1. Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutulinda na kutufikisha salama siku ya leo tunapohitimisha Mkutano wa Tano wa Bunge lako Tukufu tuliouanza tarehe 1 Novemba, 2016.
2. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kukupa pole, kwa msiba mzito uliotokea tarehe 7 Novemba, 2016 ambao Bunge lako tukufu, Serikali na Taifa tumepata kwa kumpoteza Mheshimiwa Samwel Sitta, mmoja wa Viongozi mahiri wa Bunge hili katika historia ya nchi yetu. Msiba uliotupata wa aliyekuwa Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa (2005-2010) na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Urambo Mkoani Tabora ni pigo kwa Taifa letu. Nasi Wabunge kwa kuwawakilisha Watanzania leo hii muda mfupi ujao tutaaga mwili wa kipenzi chetu Mheshimiwa Samuel Sitta. Tunamwomba Mwenyezi Mungu ailaze Roho ya Marehemu mahali pema Peponi. Amina.
3. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kutoa pole kwa mjane wa marehemu, Mheshimiwa Margareth Simwanza Sitta, Mbunge mwenzetu, watoto wake na wanafamilia wote na marafiki wote kwa ujumla kutokana na msiba mzito uliowapata. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape subira katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na siku zote wamtangulize Mwenyezi Mungu katika kuwaongoza wanafamilia waliobakia.
Sina budi kukiri kuwa Taifa limempoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na maendeleo. Enzi za uhai wake, Marehemu Mheshimiwa Sitta, alibahatika kufanya kazi na Marais wa awamu zote nne zilizopita tangu ya kwanza ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akiwa Mbunge kwa miaka 30. Alikuwa ni Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nyadhifa nyingine alizowahi kushika ni pamoja na Mkuu wa Mikoa ya Iringa na Kilimanjaro, Waziri wa Ujenzi, Waziri aliyesimamia Ustawishaji Makao Makuu, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Afrika Mashariki, Waziri wa Uchukuzi na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba.
4. Mheshimiwa Spika, tarehe 8 Novemba, 2016 tumeondokewa tena na Kiongozi wa muda mrefu Serikalini Ndugu Joseph Mungai. Kiongozi huyu ameshika nafasi mbalimbali katika utumishi wa umma ikiwemo Ubunge na Uwaziri.
5. Mheshimiwa Spika, tangu tulipokutana mara ya mwisho, pametokea majanga mbalimbali yakiwemo maradhi, ajali, na matukio mengine ambayo yamesababisha vifo na majeruhi kwa Watanzania wenzetu. Sote tunakumbuka tukio la kusikitisha la watumishi wa Serikali waliopoteza maisha wakiwa kazini walipovamiwa na wanakijiji wa Makang’wa wilayani Chamwino mkoani Dodoma. Nalaani mauaji hayo na kuvitaka vyombo vya usalama kuwachukulia hatua wote waliohusika. Vilevile, katika miezi ya Oktoba na Novemba, kumetokea ajali za barabarani katika Mikoa ya Mbeya, Pwani, Singida, Lindi, Iringa, na ile iliyopoteza ndugu zetu 19 mkoani Shinyanga na kwingineko ambako ndugu zetu walipoteza maisha. Ninatoa pole kwa wafiwa wote na wale wote waliopatwa na majanga kutokana na matukio hayo. Tunawaombea afya njema wale waliopata majeraha na waliopo hospitali. Pia niendelee kuwataka Askari wa usalama barabarani kuhakikisha wanasimamia madereva na watumiaji wa Barabara kuzingatia Sheria za usalama wa barabarani.
6. Mheshimiwa Spika, leo tunahitimisha Mkutano huu wa Tano tukiwa tumekamilisha shughuli zote zilizopangwa. Naomba nitumie fursa hii kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kukamilisha kazi zote kwa ufanisi mkubwa. Nawapongeza sana!
SHUGHULI ZA BUNGE
7. Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu tumepata fursa ya kujadili, kupokea na kushauri kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na muongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, katika kipindi hiki, tumejadili Hoja mbalimbali za Serikali ikiwemo Miswada, Taarifa za Kamati, Mkataba wa EPA, Maazimio na Kauli mbalimbali za Mawaziri. Vilevile, Wabunge walipata majibu ya maswali mbalimbali ya msingi na ya nyongeza yaliyoulizwa na Waheshimiwa Wabunge na maswali ya Papo kwa Papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
8. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pamoja na Wataalam wake, kwa kazi kubwa ya kuandaa miswada mbalimbali iliyowasilishwa katika Bunge lako Tukufu. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri. Serikali itazingatia ushauri na maoni yenu wakati wa utekelezaji.
MAAZIMIO
9. Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kupokea na kujadili Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya yaani East Africa Community – European Union Economic Partnership Agreement. Napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu mizuri tuliyoipata wakati wa mjadala wa Mkataba huo. Serikali itafanyia kazi maoni, ushauri na uamuzi wenu kuhusu Mkataba huo.
JUHUDI ZA SERIKALI ZA KUWAHUDUMIA WAATHIRIKA WA TETEMEKO LA ARDHI MKOANI KAGERA
10. Mheshimiwa Spika, mtakumbuka kuwa mnamo tarehe 10 Septemba, 2016 lilitokea tetemeko la ardhi katika eneo la Kanda ya Ziwa na hususan Mkoa wa Kagera. Tetemeko hilo lilisababisha athari mbalimbali zikiwemo vifo, majeruhi, uharibifu wa makazi na miundombinu ya umma na watu binafsi. Jumla ya Watu 117,721 wameathirika kwa kupoteza makazi yao, mali na athari za kisaikolojia katika Wilaya za Bukoba, Missenyi, Muleba, Karagwe na Kyerwa. Aidha, jumla ya watu 17 walipoteza maisha na 560 walijeruhiwa. Vilevile, nyumba 2,072 za makazi zilianguka kabisa na nyumba 14,595 za makazi zilibomoka, baadhi zina kuta au kupata nyufa kubwa na hivyo kuzifanya kuwa hatarishi kwa makazi ya binadamu. Vilevile, maafa haya yalisababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara na majengo ya Serikali 1,718 yaliyoharibika kwa viwango tofauti.
11. Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo, Serikali ilianzisha Kituo cha Operesheni na Kuratibu Maafa kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwa lengo la kuharakisha huduma. Aidha, Serikali ilitoa matibabu bure kwa majeruhi wote, kuandaa na kugharamia mazishi ya watu 17 waliofariki ambapo mimi binafsi nilihudhuria na pia kutoa mkono wa pole wa Shilingi Milioni 17 kwa wafiwa. Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali iliwahudumia wananchi walioathirika na tetemeko kwa kuwapatia misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula, madawa, nguo, makazi ya muda, vifaa vya ujenzi, vifaa tiba, vifaa vya shule na huduma ya ushauri wa kisaikolojia. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa na wadau mbalimbali walifanya Tathmini ya pamoja ya mahitaji ya haraka katika kukabiliana na Athari za Tetemeko hilo. Ambapo utekelezaji wa masuala muhimu yaliyoainishwa katika tathmini hiyo unaendelea.
12. Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha wadau, taasisi na wananchi mbalimbali kuchangia maafa hayo, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Kagera ilifungua Akaunti pekee Namba 0152225617300 katika Benki ya CRDB Bukoba yenye jina la “KAMATI MAAFA KAGERA”. Hadi kufikia tarehe 10 Novemba, 2016 kiasi cha Shilingi 5,427,671,677.32 kilikuwa kimeingizwa kwenye Akaunti hiyo. Hadi kufikia tarehe 10 Novemba 2016 Salio katika Benki ni Shilingi 4,296,038,711.79 na matumizi hadi tarehe tajwa yalikuwa ni Shilingi 1,130,428,347.53. Aidha, Kamati pia ilisajili namba za simu za mkononi za kupokea michango katika Kampuni za Vodacom (M-Pesa) 0768 196 669, Tigo (Tigopesa) 0718 069 616 na Airtel (Airtel Money) 0682 950 009 kwa jina la “KAMATI MAAFA KAGERA”. Hadi kufikia tarehe 10 Novemba, 2016, kiasi cha Shilingi 16,638,747 kilichangwa kupitia mitandao hiyo ya simu. Hivyo kufanya jumla ya fedha zilizopokelewa kupitia Benki na Mitandao ya Simu kuwa Shilingi 5,444,310,424.32. Aidha, Serikali imechangia Shilingi Billioni Moja katika kukabili janga hilo.
13. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kupokea misaada kutoka kwa Washirika wetu wa Maendeleo, Balozi na hata Nchi marafiki. Mathalan, tumepokea kutoka Serikali ya Uganda Dola za Kimarekani 200,000 sawa na Shilingi Milioni 419.2, Serikali ya India Shilingi Milioni 547, Serikali ya Kuwait Shilingi Milioni 51 na Serikali ya Uingereza iliahidi kutoa Shilingi Bilioni Sita zitakazoelekezwa kwenye ujenzi wa shule.
14. Mheshimiwa Spika, tumepokea vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 357 yakiwemo maturubai, magodoro, ndoo, mashuka, vifaa tiba, dawa na chakula kutoka Serikali za Japan, China, Kenya, Pakistan, Burundi na Rwanda.
15. Mheshimiwa Spika, taarifa ya Kikosi Kazi cha Wataalam imeainisha kuwa takribani Shilingi Bilioni 63.2 zitahitajika kurejesha hali ya kawaida katika Mkoa wa Kagera kufuatia maafa hayo. Gharama hii inajumuisha ukarabati wa shule za msingi, sekondari, vituo vya afya na taasisi nyingine katika wilaya zote sita za Mkoa huo, ujenzi mpya wa shule za Ihungo na Nyakato (tayari wafadhili wamejitolea kujenga shule hizi). Aidha, hadi kufikia tarehe 10 Novemba, 2016 kiasi cha Shilingi 966,898,826 zilitumika katika kufanya ukarabati mkubwa na mdogo wa Shule za Msingi na Sekondari pamoja na Zahanati katika Halmashauri za Mkoa wa Kagera. Serikali inaendelea na ujenzi wa Zahanati mpya (Ishozi) inayojumuisha chumba cha Upasuaji na wodi ya kinamama na watoto na usimamizi wa ujenzi wa shule za Ihungo na Nyakato. Aidha, katika kuongeza nguvu ya urejeshaji hali jumla ya Askari 96 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wakiwemo Wahandisi, Mafundi, Wapishi, na Madereva waliwasili Mkoani Kagera tarehe 19 Oktoba, 2016 kushiriki katika zoezi la kurejesha hali ya majengo na miundombinu.
16. Mheshimiwa Spika, Serikali inapenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu na wananchi kwa jumla kuwa Serikali ipo pamoja na waathirika hawa katika suala hili na ina mikakati madhubuti ya kuhakikisha tunarejesha hali bora kwa kuendelea kurudisha miundombinu, kutoa huduma za kibinadamu na matibabu kwa waathirika. Aidha, napenda kuwashukuru wale wote waliochangia katika kusaidia wenzetu wa Kagera, kwani katika kipindi hiki, tumeonesha umoja wetu, upendo wa dhati, hali ya kuthaminiana na kujaliana. Mungu awabariki sana na kuwaongezea pale walipotoa. Kipekee, niwashukuru Nchi marafiki, Balozi, Wadau wa Maendeleo wa ndani na nje ya Nchi, Taasisi za Kiserikali na zisizo za Kiserikali, Taasisi za Fedha, Kampuni, Vikundi mbalimbali, pamoja na Wananchi wote wakiwemo wale waishio nje ya Nchi.
MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2017/2018
17. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa tano wa Bunge, Serikali imewasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2017/2018. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri iliyotolewa wakati wa kujadili Hoja hiyo. Maoni na ushauri uliotolewa utazingatiwa wakati wa maandalizi ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/2018.
TAARIFA ZA KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE ZA PAC NA LAAC KUHUSU HESABU ZILIZOKAGULIWA KWA MWAKA 2013/2014 NA 2014/2015
18. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge za PAC na LAAC kuhusu Hesabu za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Serikali za Mitaa zilizokaguliwa kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni, 2014 na tarehe 30 Juni, 2015. Serikali imepokea michango na Hoja za Waheshimiwa Wabunge na itazifanyia kazi.
19. Mheshimiwa Spika, napenda kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 hadi 2016, Serikali imetakiwa kuchukua hatua kali na za haraka kwa wale wote watakaobainika kujihusisha na ubadhirifu
na wizi wa mali ya umma, ukiukaji wa maadili ya Utumishi wa Umma na wale wanaoendeleza vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya fedha za Umma. Kutokana na maelekezo hayo, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuimarisha udhibiti wa matumizi ya Serikali na kuchukua hatua kwa Watumishi wa Umma wasiozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za matumizi ya Fedha za Umma. Maafisa Masuuli wote wanakumbushwa kuzingatia kikamilifu Sheria ya Ununuzi wa Umma na Kanuni zake. Aidha, Maafisa Masuuli wote wanatakiwa kuchukua hatua stahiki za kinidhamu na kisheria kwa Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi za Serikali wanaofanya malipo yenye mashaka wakati wa kufanya manunuzi ya Umma au kuingia Mikataba na Zabuni tata za utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hatua hizo zitapunguza na kuondoa Hoja za ukaguzi na kuimarisha usimamizi wa fedha za walipa kodi.
SEKTA YA KILIMO
Mwenendo wa Uzalishaji wa Mazao Katika Msimu wa Mvua za Vuli
20. Mheshimiwa Spika, naomba nitoe taarifa kutoka Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa kuwa, kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2016 imeonesha kuwa katika maeneo mengi ya nchi, mvua zinatarajiwa kuwa chache, kuchelewa kuanza na mahali pengine kunyesha kwa mtawanyiko usioridhisha. Aidha, kwa maeneo yanayopata mvua za vuli zikiwemo Wilaya za Kyerwa, Missenyi na Karagwe, mvua zilipoanza kunyesha zilikuwa chini ya wastani na kusababisha baadhi ya mazao yaliyopandwa kuathirika. Vile vile, taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA zinaeleza kuwa katika maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua zinazoanza mwezi Novemba hadi Aprili, mvua zitachelewa na kunyesha chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi isipokuwa katika baadhi ya maeneo ya Mtwara Lindi na Ruvuma. Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwataka wataalam wa kilimo kuhakikisha wananchi katika maeneo yatakayopata mvua kidogo wanawezeshwa kupata mbegu za mazao yanayostahimili ukame na zinazokomaa haraka.
Aidha, niwashauri wakulima kuandaa mashamba yao mapema na kutumia mbegu hizo zinazokomaa mapema na kustahimili ukame. Niwasihi wananchi na wakulima kuendelea kutumia kwa uangalifu na kuhifadhi akiba ya chakula walichovuna au kununua kwa matumizi katika kaya zao. Nitoe wito kwa Sekta binafsi kuendelea kushiriki katika kutoa masoko ya kununua na kuuza mazao katika maeneo yenye ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba.
Usambazaji wa Pembejeo za Zao laTumbaku
21. Mheshimiwa Spika, ili kuondoa kero ya upatikanaji wa pembejeo kwa zao la tumbaku kwa msimu wa 2016/2017, Serikali imebadili utaratibu kutoka ule uliohusisha zabuni kwa wauzaji wa kati (middlemen) na kuweka utaratibu mpya unaohusisha wazalishaji wa pembejeo kuzisafirisha pembejeo hizo hadi katika Vyama vya Msingi vya Ushirika moja kwa moja kwa bei ya Dola za Kimarekani 40.45 kwa mfuko wa NPK (ikilinganishwa na Dola za Kimarekani 52.7 za msimu uliopita), na Dola za Kimarekani 21 pungufu kwa mbolea aina ya Urea na CAN kwa tani moja ukilinganisha uliopita. Hadi sasa wazalishaji wawili wa mbolea za tumbaku (Kampuni ya Yara Tanzania na Rosier) wamechukua jukumu hilo. Napenda kuchukua fursa hii kuvitaka Vyama vya Ushirika kusimamia kikamilifu mpango huu ili wakulima wazalishe kitaalamu na kuongeza tija katika uzalishaji.
SEKTA YA VIWANDA NA UWEKEZAJI
22. Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 17 Oktoba, 2016, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji alizindua rasmi matokeo ya Sensa ya Uzalishaji Viwandani ya mwaka 2013 iliyofanyika kwa ushirikiano wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS). Zoezi la sensa hii lilitumia taarifa za uzalishaji za viwanda za mwaka, 2013, yaani viwanda vilivyokuwepo mwaka 2013 na vilivyokuwa vinazalisha. Zoezi la ukusanyaji wa taarifa za uzalishaji, za viwanda lilifanyika mwaka 2014 na mwaka 2015 ilikuwa ni kufanya uchambuzi wa kitalaamu na kuandika ripoti.
23. Mheshimiwa Spika, matokeo ya Sensa hiyo yanaonesha kuwa, kufikia mwaka 2013 Tanzania ilikuwa na jumla ya viwanda 49,243 ambapo viwanda vidogo vinavyoajiri mtu 1 – 4 vilikuwa ni Asilimia 85.13, viwanda vidogo vyenye watu 5 – 49 ni Asilimia 14.02, viwanda vya kati vyenye watu 50 – 99 ni Asilimia 0.35 na viwanda vikubwa vyenye watu kuanzia 100 na kuendelea ni Asilimia 0.5. Hivyo, Asilimia 99.15 ya viwanda vyote nchini ni viwanda vidogo.
24. Mheshimiwa Spika, katika utafiti wa mwaka jana ilionekana kuwa mpaka mwezi Oktoba, 2015 kulikuwa na viwanda 52,579. Aidha, kwa kipindi cha mwaka mmoja tu, yaani kuanzia Novemba, 2015 mpaka Oktoba, 2016 jumla ya viwanda vipya 1,843 vimeanzishwa na kufanya jumla ya viwanda vyote nchini kufikia 54,422. Ni matumaini ya Serikali kuwa kutokana na juhudi za uhamasishaji zinazofanyika, kasi ya uanzishwaji viwanda na hasa viwanda vidogo na vya kati na vikubwa itaongezeka sana.
25. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara mbalimbali za Kisekta tayari imebainisha maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuchochea uwekezaji kama vile kuendeleza eneo la Mji wa Kigamboni na kutenga maeneo maalum ya Uwekezaji katika Mikoa mbalimbali Nchini. Hatua nyingine ni kuboresha miundombinu kama vile barabara na reli. Mfano mzuri ni ujenzi wa reli yenye urefu wa kilomita 4 katika kiwanda kipya cha KILUA GROUP cha kutengeneza nondo kilichopo Mlandizi, Pwani. Pia, Serikali inaendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika. Kwa viwanda ambavyo vipo karibu na bomba la gesi watasaidiwa kuunganishwa na gesi. Vilevile, Serikali, imechukua hatua madhubuti za kuharakisha upatikanaji wa ardhi ambacho ni kivutio muhimu katika kuhamasisha uwekezaji.
Uongezaji Kasi ya Uwekezaji kwenye Sekta ya Viwanda Nchini
26. Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kasi ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda inaongezeka ili ichangie Asilimia 15 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2020 Ili kutekeleza adhima hiyo hatua zifuatazo zinaendelea kuchukuliwa:-
Kwanza: Kutambua sekta za kipaumbele kwa kuzingatia viwanda vinavyotumia malighafi za ndani, na hususan kwenye sekta za kilimo na maliasili ili kuchochea uzalishaji vijiini na kuongeza ajira; viwanda vinavyotumia malighafi za ndani ambazo si za kilimo kama vile madini na kemikali; na kuweka msukumo kwenye kuanzisha viwanda visivyotumia malighafi za ndani kama vile uunganishaji wa magari na uzalishaji wa vifungashio.
Pili: Kuandaa Mpango mahsusi wa uwekezaji kwenye viwanda kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mpaka sasa, Mifuko ya LAPF, PPF, PSPF, NSSF na GEPF tayari wameainisha miradi ya uzalishaji watakayoanza nayo.
Tatu: Kuhamasisha Sekta Binafsi, ya ndani na nje ya Nchi, kuwekeza kwenye viwanda. Kupitia makongamano ya biashara na uwekezaji nchi mbali mbali zimehamasishwa kuwekeza nchini. Baadhi ya nchi hizo ni China, Oman, Vietnman, Urusi, Morocco n.k.
Nne: Kuingia makubaliano ya ushirikiano na Nchi zingine ili kuongeza uwekezaji. Mpaka sasa Nchi ya China imechagua jimbo la Jiangsu kuleta viwanda nchini na pia kupitia Jukwaa la Ushirkiano la China na Afrika itawezesha ujenzi wa miundombinu ikiwemo Bandari ya Bagamoyo. Aidha, kwa utaratibu huu Serikali tayari imeanza utekelezaji wa mradi wa kuunganisha matrekta 2400 pale TAMCO Kibaha kufuatia ushirikiano na Serikali ya Poland, uunganishaji wa magari wa Kampuni ya Kitanzania ya SIMBA MOTOR kwa ushirikiano na Jeshi (NYUMBU) na Kampuni ya China. Vile vile, India kupitia mradi wake wa kuimarisha uwekezaji Afrika (SITA) inasaidia utekelezaji wa mikakati minne ya kukuza na kuendeleza alizeti, pamba, ngozi na mazao ya jamii ya kunde.
Tano: Kutoa elimu na mwongozo kwa Serikali ngazi ya Mikoa na Wilaya kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika maeneo yao. Serikali imegawa Mikoa katika makundi manane ambayo Watendaji Waandamizi wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji watakwenda kuzungumza na wadau ili kuhakikisha viwanda vinasambaa Nchi nzima.
27. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu hili mambo muhimu ambayo Mikoa inatakiwa kuzingatia ni pamoja na Mikoa kuweza kubaini fursa walizonazo na kuandaa taswira ya mkoa kutegemeana na fursa walizonazo. Aidha, Mikoa inahimizwa kuhamasisha wananchi juu ya uwekezaji. Vilevile, Viongozi wa Mkoa wanashauriwa kuongeza kasi ya kuhamasisha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga maeneo na kuhakikisha kuwa wanazingatia katika mipango ya Halmashauri za wilaya ujenzi wa miundombinu wezeshi kwenye maeneo watakayotenga kwa ajili ya uwekezaji.
SEKTA YA ELIMU
Matokeo ya Mitihani ya Darasa la Saba 2016
28. Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba, 2016 Baraza la Mitihani la Taifa lilitangaza matokeo ya Mitihani wa Darasa la Saba kwa mwaka 2016. Taarifa hiyo ilibainisha kuwa katika mtihani huo, kati ya wanafunzi 789,479 waliofanya mtihani, jumla ya wanafunzi 555,291 walifaulu sawa na Asilimia 70.36. Kati yao wasichana ni 283,751 na wavulana ni 271,540. Nitumie fursa hii kuwapongeza wanafunzi wote waliofaulu na Shule zote zilizofanya vizuri na hasa wale kumi bora. Napenda kuwaagiza Viongozi wa Mikoa na Halmashauri kuendelea kukamilisha miundombinu ya vyumba vya madarasa na miundo-mbinu mingine ili kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwezi Januari, 2017. Kila Mkoa uweke lengo la kuhakikisha Wanafunzi wote watakaochaguliwa wanajiunga na Sekondari. Serikali kwa upande wake itahakikisha inatoa ruzuku kwa ajili ya mahitaji ya Wanafunzi watakaojiunga na Sekondari.
Mwenendo wa utoaji wa mikopo
29. Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 1994 Serikali ilipoanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu, jumla ya kiasi cha Shilingi Trilioni 2.44 kimekwishatolewa. Jumla ya wanafunzi 324,994 wamenufaika na fedha hizo.
30. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017 jumla ya wanafunzi 64,441 wamedahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu na orodha yao kuwasilishwa Bodi ya Mikopo ya Elimu Juu. Kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia tarehe 3 Novemba, 2016, wakati akitoa kauli ya Serikali Bungeni kuhusu upangaji na utoaji wa Mikopo ya Elimu ya Juu, ni kwamba hadi kufikia tarehe 2 Novemba, 2016 jumla ya wanafunzi 25,228 wa mwaka wa kwanza walikuwa wamekwishapewa fedha za mikopo. Kati ya wanafunzi hao, 4,787 ni Yatima, 127 wenye Ulemavu na 94 ni waliosoma Sekondari kwa Ufadhili wa Taasisi mbalimbali.
31. Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kuwa wanafunzi wote wanaoendelea na masomo, ambao ni wanufaika wa mikopo na vyuo vyao vimewasilisha Bodi ya Mikopo taarifa za matokeo wameendelea kupatiwa mikopo kama ilivyokuwa katika mwaka uliopita wa masomo.
Changamoto Zilizopo za Mkopo na Utatuzi Wake
32. Mheshimiwa Spika, ili kutatua changamoto zinazojitokeza katika uratibu wa mikopo ya wanafunzi, Serikali inafanya mapitio ya mfumo wa udahili wa wanafunzi vyuoni, utaratibu mzima wa utoaji na urejeshwaji mikopo kwa lengo la kuwa na mfumo bora zaidi na kuondoa adha inayowapata wanafunzi wanapofungua vyuo kutokana na mfumo uliopo sasa. Nimeagiza kazi hii ikamilike mapema ili mapendekezo ya mfumo utakaokuwa na tija zaidi yaweze kuzingatiwa wakati wa maandalizi ya Bajeti ya 2017/2018.
SEKTA YA ARDHI
Hali ya Migogoro baina ya Watumiaji wa Ardhi Nchini:
33. Mheshimiwa Spika, nchi yetu imeendelea kukumbwa na migogoro mbalimbali ya ardhi baina ya watumiaji wa ardhi ikiwemo migogoro mikubwa baina ya wakulima na wafugaji; migororo baina ya wananchi na wawekezaji; wafugaji na hifadhi za Taifa na baina ya wakulima na baadhi ya maeneo ya hifadhi za Wilaya mbalimbali.
Juhudi na Mikakati ya Serikali ya Kuondoa Migogoro Mikubwa ya Wakulima na Wafugaji
34. Mheshimiwa Spika, migogoro ya matumizi ya ardhi baina ya Wakulima na Wafugaji imeendelea kuongezeka kutokana na ongezeko la watu na mifugo, na vijiji kutokuwa na Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi inayoainisha maeneo mahsusi kwa ajili ya Kilimo na Ufugaji. Aidha, uwepo wa mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha ukame na ukosefu wa malisho na maji katika maeneo ya wafugaji kumesababisha uhusiano hafifu baina ya jamii za wafugaji na wakulima kutokana na mifugo kuingizwa katika mashamba ya wakulima kwa mabavu.
35. Mheshimiwa Spika, migogoro hii imesababisha kuwepo kwa vitendo vingi vya uvunjifu wa amani, upotevu wa maisha ya wananchi, baadhi ya wananchi kupata vilema vya maisha, uharibifu wa mali, uharibifu wa mazingira, athari za kijamii kama watoto kushindwa kwenda shule na wananchi kushindwa kushiriki katika shughuli za maendeleo kutokana na hofu jambo linaloweza kusababisha njaa na umaskini miongoni mwa jamii na Taifa.
Hatua za kutatua migogoro mikubwa ya wakulima na wafugaji
36. Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na migogoro na kuwawezesha wakulima na wafugaji kuendelea na shughuli zao bila migogoro, Serikali inaendelea kutekeleza mikakati ya kuainisha, kupima, kutenga na kumilikisha ardhi kwa ajili ya wafugaji na wakulima; na kanda za malisho kwa wafugaji wakubwa na wadogo itakayohusisha vijiji, Wilaya na Mikoa. Maeneo haya yatakayotengwa yatalindwa kwa kuyatangaza kwenye Gazeti la Serikali, na matumizi yake yatasimamiwa ili kuhakikisha wanafuga kwa kuzingatia uwiano wa malisho na mifugo.
37. Mheshimiwa Spika, mikakati hiyo ni pamoja na kuzigawanya Ranchi zilizopo katika vitalu ili wafugaji wenye ng’ombe zaidi ya 200 wahamie huko, kila kitalu kimoja kulingana na uwezo wa kitaalamu wa kulisha idadi maalum ya ng’ombe. Wafugaji wenye mifugo chini ya 200 watagawiwa maeneo katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili yao katika vijiji na watakuwa wanauza mifugo yao katika minada ambapo wafugaji kutoka Ili katika ranchi watafika kununua mifugo hapo. Kwa mikoa ambayo haina Ranchi za Taifa, watatenga maeneo yaliyo wazi kwa ajili ya wafugaji wakubwa.
38. Mheshimiwa Spika, ili kuzuia wafugaji kuhamahama kutafuta maji na huduma nyingine, Serikali kwa kushirikiana na wafugaji itaweka miundombinu ya majosho, mabwawa ya kunyweshea maji, huduma za ugani zikiwemo matibabu, elimu ya kulima malisho, unenepeshaji, uwekaji sahihi wa chapa za ng’ombe n.k.
39. Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua hizo, jawabu la kudumu la migogoro hii ni kuhakikisha kuwa tunawawezesha wafugaji kuvuna na kupunguza mifugo bila kupata hasara, kupitia uwekezaji wa Viwanda vya Kuchakata Nyama na Usindikaji Maziwa ili kuongeza thamani. Wizara husika zikae pamoja na kubuni Mikakati na Mipango ya kuvutia wawekezaji katika eneo hili katika miaka mitatu ijayo kuwe na tofauti.
40. Mheshimiwa Spika, aidha napenda kuzikumbusha Halmashauri za Wilaya kote nchini kuendelea kuweka na kutekeleza mipango madhubuti ya matumizi bora ya ardhi, na wale wenye Benki ya Ardhi wagawe kwa busara kwa wafugaji, wazuie wafugaji wengine wasiendelee kuingiza mifugo katika maeneo ya kilimo na watumie sheria ndogo zilizopo na kama hazipo ziandaliwe na kutumiwa; na ikibidi wahalifu wapelekwe mahakamani. Aidha, niwakumbushe wafugaji wote kufuata sheria na kwamba Serikali haitasita kuwachukulia hatua wafugaji watakaoingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima kwa makusudi.
SEKTA YA NISHATI
Mradi Kabambe wa Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Pili
41. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa nishati ya umeme, Serikali imeendelea kutoa mkazo katika kutekeleza na miradi mikubwa ya uzalishaji na usafirishaji umeme pamoja na miradi ya kusambaza umeme vijijini. Ili kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi wengi, hususan waishio vijijini, Serikali kupitia REA imeendelea kutekeleza Mradi Kabambe wa Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Pili tangu mwaka 2014. Mradi huu unatekelezwa katika wilaya zote za Tanzania Bara. Hadi kufikia Oktoba, 2016 ujenzi wa kilometa za njia ya msongo wa Kilovolti (kV) 33 umefikia Asilimia 95.6; ujenzi wa kilometa za njia ya Msongo wa Volti 400 umefikia Asilimia 89.3; na ufungaji wa transfoma umefikia Asilimia 87.2. Aidha, jumla ya wateja 146,311 wa awali sawa na Asilimia 59 ya lengo la wateja 255,000 wameunganishiwa umeme kupitia mradi huo.
Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu
42. Mheshimiwa Spika, Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 5 katika vijiji 7,873 vya wilaya zote za Tanzania Bara. Takriban vijiji 7,697 vitapelekewa umeme wa gridi ya Taifa na vijiji 176 umeme wa nje ya gridi (Off-grid). Mpango huu utaongeza wigo wa usambazaji umeme katika maeneo ambayo hayakufikiwa na miradi ya REA Turnkey Phase I na II. Ili kutekeleza miradi hiyo kwa kasi zaidi, Serikali ya Awamu ya Tano katika bajeti yake ya mwaka 2016/17 iliongeza fedha za kupeleka umeme Vijijini kutoka Shilingi Bilioni 357.117 zilizotengwa mwaka 2015/16 hadi Shilingi Bilioni 587.61 mwaka 2016/17. Hadi kufikia mwezi Oktoba, Serikali imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 109.8 kwa ajili ya Mfuko wa Nishati Vijijini kutoka kwenye vyanzo vya fedha za ndani. Kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 100.4 ni tozo ya mafuta na Shilingi Bilioni 9.4 ni tozo ya umeme.
43. Mheshimiwa Spika, zabuni za kupata wakandarasi wa kutekeleza mradi huu zilitangazwa tarehe 1 Agosti, 2016. Kwa sasa REA inaendelea na uchambuzi wa zabuni hizo. Taratibu zote za mradi huo zimepangwa kukamilika mwezi Januari, 2017. Natoa rai kwa viongozi mbalimbali wa Serikali wakimemo Waheshimiwa Wabunge kuwahamisha wananchi katika maeneo yao kutumia fursa ya kuunganishiwa umeme wakati wakandarasi wakiwa kwenye maeneo ya miradi. Katika kipindi hicho bei ya kuunganisha umeme ni Shilingi 27,000 tu kama ilivyotaarifiwa awali katika Bunge hili.
44. Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeanzisha Mradi wa Kupanua Wigo wa Upatikanaji wa Umeme Vijijini (Tanzania Rural Electricity Expansion Project). Mradi huo utagharamiwa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia wa Dola za Kimarekani milioni 209. Mradi ulizinduliwa tarehe 26 Agosti 2016, katika kijiji cha Kwedikwazu wilayani Handeni Mkoani Tanga na utawezesha kaya takriban 500,000 kupata huduma ya umeme nchini.
SEKTA YA MADINI
Migodi Mikubwa Kuendelea Kulipa Mrabaha
45. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kati ya Oktoba, 2015 na Oktoba, 2016 Serikali ilifanya ukaguzi na kuwezesha migodi mikubwa kulipa mrabaha ambapo: Migodi Mikubwa ya Dhahabu ya Biharamulo, Bulyanhulu, Buzwagi, Geita, New Luika na North Mara imelipa kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 69.4 ikiwa ni Mrabaha, sawa na Shilingi Bilioni 151.4. Vilevile, Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka umelipa kiasi cha Dola za Kimarekani 309,836 na Shilingi Milioni 676 ikiwa ni mrabaha. Aidha, Mgodi wa TanzaniteOne umelipa mrabaha wa Dola za Kimarekani 189,731 sawa na Shilingi Milioni 414.
Kuhamasisha Masoko ya Madini ya Vito Nchini
46. Mheshimiwa Spika, Serikali iliandaa mnada wa madini ya vito, hususan tanzanite uliofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 12 Agosti, 2016 Jijini Arusha. Katika mnada huo madini yenye thamani ya Dola za Kimarekani 3,448,050, sawa na Shilingi Bilioni 7.56, yaliuzwa na kuwezesha Serikali kukusanya Dola za Kimarekani 150,491.06, sawa na Shilingi Milioni 331 ikiwa ni mrabaha kutokana na madini yaliyouzwa.
47. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kusimamia Sekta za Nishati na Madini ili ziweze kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.
TAARIFA YA MAKUSANYO YA FEDHA KWENYE HALMASHAURI KWA MWAKA 2016/2017
48. Mheshimiwa Spika, katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 Halmashauri ziliidhinishiwa kukusanya mapato ya Shilingi Bilioni 665.4. Hadi kufikia Septemba, 2016 Halmashauri zimekusanya Shilingi Bilioni 114.46, sawa na Asilimia 17.2 ya makisio. Kiwango hiki cha ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri bado hakiridhishi. Hivyo, naomba nitumie fursa hii kuhimiza Halmashauri zote nchini kuongeza jitihada katika kukusanya mapato ya vyanzo vya ndani. Nazihimiza Halmashauri kutumia mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji mapato na pia katika maeneo ya kutolea huduma za afya ili kudhibiti upotevu wa mapato. Aidha, naelekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa waimarishe mifumo ya udhibiti wa ndani na kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana katika kila huduma au bidhaa inayonunuliwa na Halmashauri. Halmashauri hazina budi kuepuka matumizi ya fedha yasiyo na tija katika shughuli za uendeshaji wa Mamlaka hizo.
49. Mheshimiwa Spika, Halmashauri zote zinaagizwa zifuatilie kwa karibu mapato na matumizi ya fedha zinazopelekwa kwenye shule na kwenye vituo vinavyotoa huduma za afya ikiwemo Hospitali, vituo vya afya na zahanati. Ili kufikia azma hiyo, uwekwe utaratibu madhubuti wa ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha hizo kwa kushirikisha Wakaguzi wa ndani wa Halmashauri.
MAONI NA MAPENDEKEZO KUHUSU TAARIFA YA KAMATI YA BUNGE YA LAAC
50. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ushauri mzuri na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya LAAC kuhusu ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2013/2014 na 2014/2015, Serikali imeshatoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa zinatekeleza kwa ukamilifu maelekezo yote ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa na Kamati nyingine ili kuondoa hoja zilizojitokeza katika taarifa ya CAG. Aidha, Halmashauri zinaelekezwa kuimarisha mifumo ya uthibiti wa ndani na kutumia vizuri ushauri unaotolewa na Kamati za Ukaguzi ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma.
51. Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kwamba Halmashauri zote ni lazima zitekeleze vipaumbele vilivyoidhinishwa katika mpango na bajeti kwa mwaka 2016/17 kwa kupanga vema utekelezaji kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha. Halmashauri ziendelee kuimarisha usimamizi wa mikataba ili thamani ya fedha za Serikali iweze kupatikana katika miradi na Kandarasi nyingine zilizoingia Mikataba na Halmashauri.
HITIMISHO
52. Mheshimiwa Spika, wakati tunahitimisha mkutano huu leo, napenda nitumie nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kusimamia vizuri na kwa weledi mkubwa vikao vyote vya mkutano huu. Niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu. Ninashukuru pia Watendaji wa Serikali kwa kuwasaidia Mawaziri na Naibu Mawaziri katika kujibu maswali na hoja mbalimbali za Wabunge. Niwashukuru wanausalama wote kwa kazi yao nzuri. Niwashukuru madereva wote kwa kuwaendesha Mawaziri, Wabunge na Watendaji wote kwa usalama kabisa. Niwashukuru pia wanahabari wote kwa kuihabarisha jamii juu ya mkutano wetu. Kipekee, nimshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililah na timu yake kwa kutuwezesha kukamilisha shughuli zote za mkutano huu kwa mafanikio makubwa.
53. Mheshimiwa Spika, mwisho, lakini si kwa umuhimu, nitumie muda huu kumwomba Mwenyezi Mungu awalinde na awaongoze Waheshimiwa Wabunge wote katika safari ya kurejea majumbani kwenu. Aidha, nawatakia kila la kheri na fanaka katika sikukuu zijazo za mwisho wa mwaka na kuwatakia mwaka mpya wa 2017.
54. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 31 Januari, 2017, siku ya Jumanne, saa 3:00 asubuhi litakapokutana katika ukumbi huu hapa Dodoma.
55. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.