Mbwana Samatta atoswa tuzo za Mchezaji Bora Afrika CAF
Nahodha wa timu ya taifa Tanzania, Mbwana Samatta ametoswa kwenye mbio za kuwania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Afrika Pierre-Emerick Aubameyang, Mahrez na Sadio Mane wakizidi kung’ara.
Shirikisho la Soka Afrika, CAF limetangaza orodha ya majina ya wachezaji waliotinga tano bora kuwania tuzo ya mchezaji bora wa Afrika mwaka 2016, jina la mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samatta halipo katika orodha ya wachezaji hao waliofanikiwa kuingia tano bora.
Samatta alikuwepo kwenye orodha ya awali, lakini safari hii alikuwa akiwania tuzo ya mchezaji bora Afrika kwa ujumla baada ya msimu uliopita kushinda tuzo ya mchezaji bora Afrika kwa wachezaji wa ndani wakati akiitumikia klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Nahodha huyo wa Stars anaecheza klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji ameshindwa kusonga kwenye kinyang’anyiro hicho kutokana na ushindani mkubwa kutoka kwa vipanga wanaocheza kwenye klabu kubwa na maarufu duniani za Bundesliga, Ligi Kuu Uingereza, na Serie A.
Mchezaji bora wa mwaka wa Afrika ni wafuatao;
1. Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon & Borrusia Dortmund)
2. Riyad Mahrez (Algeria & Leicester City)
3. Sadio Mane (Senegal & Liverpool)
4. Mohamed Salah (Egypt & Roma)
5. Islam Slimani (Algeria & Leicester City)
Mchezaji bora wa Afrika (Ligi za ndani ya Afrika), tano bora ni hawa wafuatao;
1. Khama Billiat (Mamelodi Sundowns & Zimbabwe)
2. Keegan Dolly (Mamelodi Sundowns & South Africa)
3. Rainford Kalaba (TP Mazembe & Zambia)
4. Hlompho Kekana (Mamelodi Sundowns & South Africa)
5. Denis Onyango (Mamelodi Sundowns & Uganda)
Kwa hatua ya mwisho, kura kutoka kwa Makocha wakuu/Wakurugenzi wa ufundi wa mashirikisho 54 yanayotambuliwa na CAF pamoja na wajumbe washiriki, Visiwa vya Reunion na Zanzibar pamoja na nusu ya paneli ya wajumbe 20 (watu 10) zitahesabiwa kuwafahamu washindi.
Tuzo hizo za 2016 za Glo-CAF zinazodhaminiwa na kampuni ya mawasiliano, Globacom zitafanyika Alhamisi, Januari 5, 2017 mjini Abuja Nigeria.