Mrisho Ngasa asajiliwa Mbeya City
Mwezi Septemba mwaka huu Ngasa alijiunga na Fanja FC inayoshiriki ligi kuu nchini Oman (Oman Professional League) ikiwa ni wiki tatu tu, baada ya kuvunja mkataba na klabu ya Free State Stars ya South Africa.
Nyota huyo wa zamani wa vilabu vya Kagera Sugar, Yanga, Azam FC na Simba vyote vya VPL hajadumu Oman na hatimaye amerejea tena nchini na kusajiliwa na klabu ya Mbeya City ambapo ataungana na kocha wake wa zamani Kinna Phiri aliyemsajili kutoka Yanga kwenda Free State Stars kabla ya kocha huyo kutimuliwa kufatia mfululizo wa matokeo mabovu.
Afisa habari wa Mbeya City Dismas Ten ame-post picha kwenye ukurasa wake wa Instagram akiwa pamoja na Mrisho Ngasa na kuandika maneno yanosomeka: “Mnapokamilisha jambo kutakiana heri ndio uungwana. Kila la heri anko @mrisho_ngasa_17.”
Habari za Ngasa kujiunga na Mbeya City zilianza tangu aliporejea nchini akitokea South Africa baada ya kuvunja mkataba na Free State lakini ghafla akaibukia Oman na kusajiliwa na Fanja FC siku chache baada ya klabu hiyo kumsajili mtanzania mwingine Danny Lyanga mshambuliaji wa zamani wa Simba.
Jana jioni zikaenea tena habari kwamba Mbeya City wameshakamilisha usajili wa Ngasa. Lakini uongozi wa klabu hiyo haukuwa tayari kuthibitisha badala yake ukasema utatoa taarifa rasmi, mwisho wa siku raundi ijayo ya VPL Ngasa atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaokipiga Mbeya City.