Reli ya Standard Gauge kutoka Dar mpaka Mwanza kuanza kujengwa Disemba, 2016

Hatua ya kwanza ya maandalizi ya ujenzi wa reli ya Standard Gauge imeshaanza ambapo awamu ya kwanza ya ujenzi huo kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza itaanza rasmi Disemba 6, 2016.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO) Masanja Kadogosa amesema serikali imetenga trilioni 1 kwa ajili ya ujenzi huo.

“Ujenzi wa reli ya standard gauge umeshaanza lakini hatua iliyokuwepo haionekani, tenda zimeshaanza kutangazwa,”alisema Kadogosa wakati akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Alisema ujenzi huo utaanza kwa awamu na kwamba awamu ya kwanza inatarajiwa kuanzwa Disemba 6, 2016 wakati ya pili itaanza Februari 15, 2016.

“Ujenzi huo utachukua miaka mitatu kukamlika, ambapo utaleta manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho. Pia utarahisisha usafirishaji wa mizigo kutokana na kwamba litakuwa na mabehewa yenye kilomita 2 ambayo sawa na ukubwa wa malori 300,” alisema.

Alisema wamiliki wa majengo yatakayo athiriwa na ujenzi huo watalipwa fidia.
“Hifadhi ya reli ina maana kwamba kila upande inaachwa mita 30, hivyo kama kuna nyumba zitakazokuwa nje ya mita hizo zitatakiwa kubolewa wamiliki watalipwa fidia,” alisema.

Aidha, Kadogosa alisema kuna miradi mingine midogo ya ujenzi na ukarabati itafanyika ikiwemo ya ujenzi wa reli mpya ya Dar es Salaam ambayo itatumiwa kwa ajili ya usafiri kwa wakazi wa jiji hilo.

“Kuna Mradi wa kujenga reli mpya katika jiji la Dar es Salaam na viunga vyake kwa ajili ya treni za abiria ili kupunguza msongamano wa abiria na magari. Mradi huu uko katika hatua ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali chini ya kampuni ya ushauri ya GIBB Engineering ya Afrika Kusini na kwamba inatarajiwa kukamilika Disemba 2016,” alisema.