Sakata na kifo cha Faru John (38), limechukua sura mpya,kaburi la Faru John layeyuka


Sakata na kifo cha Faru John (38), limechukua sura mpya baada ya wahifadhi wa eneo la Sasakwa Singita Grumet kueleza kuwa hakuna kaburi lake kwa kuwa hakuzikwa.

Wamesema hayo siku moja baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutangaza kuunda timu mpya kuchunguza mazingira ya kifo cha faru huyo huku akihoji mambo manne yaliyozua utata.

Mambo aliyohoji wakati akifanya majumuisho ya ziara yake mkoani Arusha ni juzi, Faru John aliumwa lini, aliumwa nini, daktari gani aliyemtibu na zilipo taarifa za matibabu yake.

Pia aliagiza mwili wa faru huyo kufukuliwa na kutazama kama vinasaba vyake vinaendana na watoto wake 26 ambao bado wapo katika Creta ya Ngorongoro.

Akizungumza na mwandishi wetu jana, mmoja wawahifadhi wa Sasakwa Grumet aliyeomba kutotajwa jina ili kutoathiri uchunguzi wa tukio hilo, alisema kitaalamu wanyama ambao wanakufa bila kuwa na magonjwa ya mlipuko katika maeneo ya hifadhi hawazikwi. “Faru John baada ya kufa aliondolewa pembe zake na kutupwa ili kiwe chakula cha wanyama wengine wanaotegemea mizoga, lakini kuna mifupa yake,” alisema.

Alisema faru huyo aliombwa na Grumet kwenda kupanda faru waliopo katika eneo hilo, hasa baada ya dume aliyekuwapo huko kuuliwa na tembo. “Baada ya kuonekana kuna haja ya kutafuta dume, ndipo tuliomba kupata faru dume na tukaletewa na baadaye alikufa,” alisema.

Eneo hilo la Sasakwa Singita Grumet ni mali ya mfanyabiashara mkubwa raia ya Marekani, bilionea Tudor Jones ambaye amewekeza katika maeneo kadhaa ya uhifadhi.

Akifafanua hatua zinazochukuliwa baada ya mnyama kufa katika hifadhi, mhifadhi Peter Isango alisema kwa kawaida huzikwa au kuchomwa moto pale tu wanapobainika kuwa na magonjwa kama kimeta. “Kama mnyama ana magonjwa ambayo yanaweza kuambukiza, basi anachomwa moto au kufukiwa lakini kama anakufa kawaida na magonjwa ya kawaida huwa anatupwa ili fisi, bweha na wanyama wengine wanaokula mizoga wale na hii ndiyo ikolojia,” alisema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mkurugenzi mkazi wa shirika la uhifadhi la kimataifa la Frankfurt Zoological Society, Gerald Bigurube ambaye alisema kwa kawaida wanyama wanaokufa hifadhini huwa hawazikwi.
#Mwananchi