Basi la Mohammed Trans Lapata Ajali mbaya, Watu Kadhaa Wafariki Dunia
Matukio ya ajali za barabarani yameendelea kuutikisa Mkoa wa Singida baada ya abiria 10 kupoteza maisha na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa ndani ya siku tisa.
Desemba 30, mwaka jana katika Kijiji cha Tumuli Wilaya ya Iramba abiria watatu walikufa na wengine 25 kujeruhiwa na ajali nyingine ilitokea Januari Mosi katika Kijiji cha Kintukuntu wilaya humo na kuua abiria mmoja na kujeruhi watatu.
Ajali nyingine iliyohusisha bajaji ilitokea jana Januari 7 katika Barabara ya Mwankoko na kumuua dereva na abiria wawili.
Siku moja kabla ya tukio hilo, ajali ya basi la Mohammed Trans lililokuwa linatokea Tanga kwenda Shinyanga ilisababisha vifo vya abiria watatu na kujeruhi wengine watano wote wakiwa ni walimu.
Akitoa taarifa ya ajali ya basi la Mohammed Trans jana, Kaimu Kamanda Polisi mkoani hapa, Mayala Towo alisema ilitokea Januari 6, saa nne usiku katika Kijiji cha Mseko wilayani Iramba.
Kamanda huyo aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Mussa Rajabu (55), Farahan Manyama (34) na John Tungaraza (39) wote wakiwa ni walimu, wakazi wa Geita.
Pia, alisema majeruhi ambao pia ni walimu wamelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo.
Kamanda huyo aliongeza kuwa walimu hao walikuwa wametokea kwenye Chuo cha Eckenford mkoani Tanga walikokuwa wakichukua mafunzo mbalimbali. Alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva.
Towo alisema basi hilo lenye namba za usajili T 786 AWJ aina ya Scania lilikuwa linaendeshwa na Jovin Jackson (38), mkazi wa Shinyanga liligonga kwa nyuma lori lenye namba B.6705A lililokuwa likivuta tela B.0568A lililokuwa likienda Burundi.
Akifafanua, alisema dereva wa basi alitaka kulipitia lori hilo, lakini alipogundua hataweza aliamua kurudi ghafla kushoto na mwendo kasi aliokuwa nao alijikuta analigonga lori hilo kwa nyuma.
Towo alisema baada ya kusababisha ajali hiyo dereva alitoroka na kukimbilia kusikojulikana. Juhudi zinaendelea kumsaka ili afikishwe mahakamani.