Marekani kumsaka mtoto wa Osama Bin Laden Aliyeapa Kulipa Kisasi
Marekani imesema kuwa imemuorodhesha mtoto wa mwisho wa Osama Bin Laden, Hamza, katika orodha ya magaidi wanaosakwa na taifa hilo.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema kuwa Hamza Bin Laden ameanza kushiriki katika maswala ya kundi la al Qaeda, kundi la jihad lililofadhiliwa na babake.
Hamza amesema kuwa atalipiza kisasi mauaji ya babake yaliotekelezwa na kikosi maalum cha Marekani kwa kutekeleza mashambulizi dhidi ya Wamarekani.
Hamza amepigwa marufuku kufanya biashara na raia wa Marekani huku mali zake zikizuiliwa pia.
Mamake Hamza ni Khairiah Sabar, mmoja wa wake za Osama aliyekamatwa wakati wa shambulio la wanajeshi wa Marekani kwenye maficho ya Osama mjini Abbotabad nchini Pakistan mwaka 2011.
Mkuu wa kitengo cha usalama cha kundi la al-Qaeda Ibrahim al-Banna pia ameongezwa katika orodha hiyo .
Marekani imetoa kitita cha dola milioni 5 kwa mtu yeyote atakayemkamata al-Banna.
Hamza bin Laden alitambuliwa kuwa mmoja wa viongozi wa al-Qaeda mwaka 2015 na baadaye akaapa kulipiza kisasi mauaji ya babake mwezi Julai mwaka uliopita.
Katika ujumbe wa sauti wa dakika 21 wenye kichwa "We Are All Osama," (Sote ni Osama), na uliochapishwa katika mitandao, aliapa lazima angelipiza kisasi mauaji ya babake mwaka 2011 nchini Pakistan.
''Tutaendelea kuwasaka na kuwapiga popote pale mtakapokuwa mmejificha ati nyuma ya pazia za usalama kwa maovu mnayoyaendeleza ,Palestina, Afghanistan, Syria, Iraq, Yemen, Somalia na kote kwenye ardhi ya waislamu mnayokalia,'' shirika la habari la Reuters lilimnukuu.
''Na kwa wale wanaodhania kuwa tutakuwa tukilipiza kisasi mauaji ya Osama ole wenu, kwanini sisi tutakuwa tukilinda dini ya kiislamu''alisema Hamza.
Hamza, kulingana na wachanganuzi, alitambulishwa na kiongozi wa kidini wa kundi la al-Qaeda Ayman al-Zawahiri katika ujumbe huo uliolenga kuwavutia vijana ambao kwa sasa wamejiunga kwa wingi na kundi la Islamic state.
Hamza sasa anaungana na nduguye wa kambo, Saad, kuwa miongoni mwa watu wa jamii ya Osama walioorodheshwa kuwa magaidi.
Chanzo: BBC
Chanzo: BBC