Waziri Mkuu apokea ugomvi wa DC ,Mbunge

Mgogoro baina ya Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia na mkuu wa wilaya hiyo, Saimon Odunga umechukua sura mpya, safari hii ukiibuka katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dodoma (RCC) ambayo imeamua ufikishwe kwa Waziri Mkuu.

Kikao hicho ambacho kilifunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kuongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana kilifanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango.

Baada ya Odunga kupewa nafasi ya kuchangia ajenda mara baada ya Majaliwa kuondoka, aliomba ushirikiano kutoka kwa wabunge ilikutekeleza shughuli za maendeleo. “Ninaomba waheshimiwa wabunge watusaidie kulisemea hili kwa sababu hali ni mbaya katika sekta nyingi,” alisema.

Akizungumza katika kikao hicho, Nkamia, ambaye aliwahi kuwa naibu waziri, alianza kwa kumuomba Rugimbana kusaidia katika sekta ya ardhi akisema ina matatizo mengi na kutoa mfano wa Wilaya ya Chemba.

Alisema katika wilaya hiyo kuna tapeli wa ardhi ambaye amesaidiwa na viongozi kupata ardhi yenye ukubwa wa ekari 500 kinyume na sheria.

Alihoji sababu za mkuu huyo wa wilaya kutaka wabunge washiriki katika kusukuma hoja mbalimbali za maendeleo, wakati anadharau wabunge, mwenyekiti wa halmashauri na viongozi wengine wa chama wilayani humo. “Huyu ni mkuu wa wilaya ambaye anaongoza kwa rekodi ya kuwakamata watu kwa kutumia madaraka yake. Nimesikia jana (juzi) kuwa na mimi nawindwa ili nikamatwe. Niko tayari kukamatwa,” alisema Nkamia, ambaye anaongoza Jimbo la Chemba kwa kipindi cha pili mfululizo. “Nakuomba mkuu wa mkoa umuite huyu dogo (DC) umkanye kuhusu hii tabia yake ya kudhalilisha watu. Kwa kuwa bwana mkubwa (DC) hapo ameanzisha vita na sisi tunaomsaidia kazi. Sisi tuna busara zetu, hatuwezi kuingia vitani,” alisema.

Nkamia alimuomba Rugimbana kuwaita wote wawili-Odunga na yeye-wakae pamoja na kutafutia suluhu ya jambo hilo ambalo alisema linaweza kukwamisha maendeleo ya jimbo hilo.

Alimuonya mkuu huyo wa wilaya kuhusu tabia ya kuwatia mbaroni wananchi wanaouliza maswali wakati ni haki yao kufanya hivyo.
#KuperuziNaKudadisi #Mwananchi