Faida ya Ukwaju kiafya mwilini



UKWAJU ni tunda lenye faida nyingi mwilini mwa mwanadamu. Tunda hili huweza kutumika kutengeneza juisi ambayo matumizi yake yana faida kubwa kwa mwanadamu

Ukwaju unapatikana kwa wingi sana sokoni. Unaweza kutengeneza juisi kwa kuandaa maji kwenye dishi na uoshe kidogo tuu baada ya kuuosha chukua ukwaju wako weka kwenye sufuria yenye maji ya saizi na injika jikoni, uache uchemke kwa dakika 10/15 ili uuwe vijidudu.

Ipua uache kwa muda upoe, andaa maji yako masafi na chujio ili uweze kuchuja juisi yako kwa uangalifu, weka sukari kwa kiasi unachopendelea (kama una kisukari weka asali) pia ili kupunguza ukali

unaweza ukaweka hiliki au vanila ili kupata ladha, weka kwenye friji na acha ipoe, tayari kwa kunywa.

Kuna faida kubwa ya juisi kwani ni chanzo kizuri cha viua sumu mwilini ‘antioxidants’ ambavyo huzuia saratani (cancer), una Vitamini B na C vilevile “carotentes,” hushusha joto la mwili na kuondosha homa, hasa homa ya malaria na homa ya matumbo.

Ukwaju huulinda mwili dhidi ya mafua na kero za mafua kooni, husaidia myeyusho na mmeng’enyo wa chakula na kuondosha kuvimbiwa.

Ukwaju husaidia kutibu matatizo ya nyongo (bile disorders), kurahisisha choo (laxative), husaidia kupunguza wingi wa lehemu (cholesterol) na hivyo kuimarisha moyo, husaidia ngozi kuwa nyororo, vilevile husaidia ngozi inayopona baada ya kuungua au yenye vidonda, pia husaidia kuua minyoo tumboni (kwa watoto wadogo).