Fumanizi: Kwanini wanawake hupenda kuwalaumu wanawake wenzao?



Huwa inatokea sana pale mwanamke anamfumania mume au mpenzi wake, kitakachotokea kama si kumpiga mwanamke aliyemfumania na mumewe, basi atamporomoshea matusi au kumlaumu sana. Si hivyo tu, hata pale mwanamke anapopata fununu kwamba mume wake au mpenzi wake anatoka na mwanamke fulani, sio kwamba atamkabili mumewe au mpenzi wake kutaka kujua ukweli wa jambo hilo, bali atakachofanya ni kumkabili mwanamke huyo iwe ni moja kwa moja au kwa kutumia wanawake wenzie ili wamfikishie ujumbe huyo mwanamke anayemtuhumu.

Je ni kwa nini hali hiyo hutokea……? 

Hapa chini nitajaribu kudadavua sababu kadhaa zinayowafanya wanawake kukimbilia kuwalaumu wanawake wenzao wanaowafumania na waume zao:
1. Kupinga kuhusu jambo hilo - Sababu kubwa inayowafanya wanawake kuwalaumu wanawake wenzao pale wanapowafumania na wenzi wao ni kwa kuwa ni rahisi zaidi kukabiliana na wanawake wenzao kuliko waume zao. Ingawa inawezekana mwanamke akawa anahisi kwamba mwenzi wake anatoka nje, lakini mara nyingi wanawake hupinga uwezekano wa jambo hilo kuwepo. Hiyo ni kwa sababu wakati mwingine mwanawake hutokea kumuamini mwenzi wake kupita kiasi, hivyo kutotaka kuruhusu mawazo ya aina hiyo yatawale kichwa chake. Hivyo basi kuwalaumu wanawake wenzao ni rahisi zaidi kuliko kujikagua na kuangalia kama mahusiano yake na mwenzi wake iwapo yana tatizo. Lakini kinyume chake huamini kwamba ni lazima mwanamke huyo ndiye aliyemshawishi mwenzi wake mpaka akakubali kutoka naye. Pia huamini kwamba kama mwanamke huyo asingejirahisisha kwa mwenzi wake, isingekuwa ni rahisi kwake kutongozwa na kukubali, ni lazima kulikuwa na aina ya kujirahisisha ili kumshawishi mwenzi wake atoke naye. Lakini pia wanawake wengi huchukulia kitendo cha mwenzi wake kutoka nje ni kama wamechokwa na sasa waume zao hawawataki. Hakuna mtu anayependa kuachwa, hivyo ni rahisi zaidi kuwakabili au kuwalaumu wanawake wenzao kuliko waume zao au hata kujilaumu kutokana na mahusiano mabovu na wenzi wao


2. Kuhisi kusalitiwa kama mwanamke - Kwa kawaida wanaume wana tabia ya, "kila mtu na lwake," tofauti na wanawake, wao wana tabia ya ushirikiano na wanaamini kwamba madhila ya mwenzake ni ya kwake pia. Hivyo kitendo cha kugundua kwamba mwanamke mwenzake amemsaliti jambo hilo humuumiza sana. Ingawa wanawake wanajua wazi kwamba mwanaume kutoka nje ni jambo rahisi na linalowezekana sana kutokana na asili ya wanaume, lakini huamini kwamba wanawake ni wamoja na hawapaswi kusalitiana wao kwa wao.

3. Kutafuta shabaha dhaifu – Baadhi ya wanawake huona ni rahisi zaidi kuwakabili wanawake wenzao kuliko waume zao. Hususan kama anamuogopa mumewe. Kama mwanaume ana historia ya unyanyasaji na upigaji wa wanawake halafu ikatokea mwanamke akagundua kwamba mwenzi wake huyo anatoka nje, kamwe haitatokea mwanamke huyo kumkabili mumewe. Kitakachotokea ni kwa mwanamke huyo kumkabili mwanamke mwenzie akiamini kwamba shari haitakuwa kubwa ukilinganisha na ya mumewe. Pia kuna baadhi ya wanaume wana tabia ya uzinzi na mkewe au mpenzi wake anajua kabisa kwamba ni vigumu kwake kubadilika. Hapa atakachofanya mwanamke huyo ni kukimbizana na wanawake wenzie anaowahisi kuwa wanatoka na mumewe au mpenzi wake huyo ili kuwapa ujumbe kwamba anawafahamu na anawafuatilia, akiamini kwamba watamwacha mumewe, hivyo haoni sababu ya kumkabili mpenzi wake.

4. Wanawake hawapendi kupoteza – Inapotokea mwanamke amegundua kwamba mpenzi wake anatoka nje, hujiwa na mawazo mengi sana, miongoni mwa mawazo hayo ni(i). Je kuna jambo amemkosea huyo mwenzi wake mpaka kufikia kiasi cha kumsaliti? (ii). Je Mwanamke huyo aliyotoka na mwenzi wake ni mzuri kiasi gani, au amemzidi na kitu gani hasa? Kama ikitokea akimkabili mwenzi wake kutaka kujua ukweli kuhusu jambo hilo halafu huyo mpenzi wake akasema hampendi huyo mwanamke na wala hamtaki ila huyo mwanamke ndio anajipendekeza kwake, hapo itakuwa ni rahisi kwake kumkabili huyo mwanamke kidudu mtu, kwani mpaka hapo atakuwa amethibitisha kwamba yeye ni mshindi kwani mwenzi wake yuko upande wake na si wa hawara yake.

5. Amepanga kuishi na mwenzi wake mpaka kifo kiwatengenishe- Kuna wanawake ambao wamejitolea na kujiapiza mioyoni mwao kwamba wao na wenzi wao wataishi pamoja labda tu kifo ndio kitawatenganisha. Hata kama itatokea ajue dhahiri kwamba mwenzi wake anatoka nje na amejitahidi kulijadili jambo hilo na mwenzi wake lakini haoneshi dalili za kuacha mchezo wake huo, basi ni rahisi sana kwa mwanamke kuhamishia hasira zake kwa wanawake anaowahisi kuwa wanatoka na mwenzi wake. Ukweli ni kwamba hakuna mwanamke anayependa kufanywa mjinga katika uhusiano, hata kama kiukweli watu waliomzunguka humwona kuwa ni mjinga kutokana na vitendo anavyofanyiwa na mwenzi wake, lakini anashindwa kuchukua maamuzi magumu. Hivyo basi ili kuondoa hiyo dhana ya kuonekana mjinga hukimbilia kuwakabili wanawake wenzie anaohisi wanatoka na mwenzi wake.

6. Anatoka na mwanamke anayemfahamu vizuri sana – Hii ni moja ya sababu nzuri inayoweza kutumiwa na mwanamke kuhalalisha kwamba ni kwa nini amkabili manamke mwenzie badala ya mwenzi wake. Kama inatokea mwanaume anatoka nje na rafiki wa karibu wa mkewe, mfanyakazi mwenzie au kibaya zaidi atoke na ndugu wa karibu, hapo ni dhahiri mwanamke anayo kila sababu ya kumlaumu mwanamke mwenzie. Na si hivyo tu kama inatokea anatoka na ndugu wa karibu labda tusema dada au mdogo wake wa kike, huwa inawaumiza sana wanawake na uwezekano wa ndugu kusambaratika ni mkubwa, kwani anashindwa kuamini kile kilichotokea. "Yaani hata ndugu yangu mwenyewe ananisaliti……" anaweza kujiuliza. Na kama ni shoga yake ndio kabisaa itamuuma zaidi. Ikumbukwe kwamba wanawake huwa wanashirikiana hisia. Kama inatokea anagundua kwamba yule rafiki aliyemuamini na ambaye anamshirikisha katika madhila yake kwa kumweleza matatizo yake na mwenzi wake, ndiye anayetoka na mpenzi wake, jambo hili huwaumiza sana wanawake kihisia