Hatua Kuu za Ugonjwa wa VVU/UKIMWI (HIV/AIDS stages) na Dalili Zake
Ugonjwa wa HIV/AIDS umekuwa janga kubwa sana duniani kwa sasa kutokana kuathiri watu wengi na kukosekana kwa tiba ya ugonjwa huu. Maambukizi ya ugonjwa wa HIV/AIDS hufahamika kama maambukizi ya VVU (Virusi vya Ukimwi). Mtu anapopata magonjwa nyemelezi (opportunistic infections) ndiyo huwa tunasema mtu amepata ugonjwa wa UKIMWI au AIDS.
Je ni kuna hatua ngapi za ugonjwa wa VVU/UKIMWI na dalili zake ni zipi?
Kwa mujibu wa uanishaji uliofanywa na wataalamu wa shirika la Afya Duniani yaani WHO, kuna hatua (stages) kuu nne za ugonjwa wa VVU/UKIMWI ambazo ni:
1. Hatua ya kwanza [Primary HIV Infection]
Hatua hii huwa kwa muda wa wiki nne. Ni asilimia 20 tu ya watu wenye maambukizi ya VVU walio kwenye hatua hii ambao hupata dalili na viashiria vikali vya ugonjwa huu lakini mara nyingi madaktari hushindwa kutambua kama mgonjwa amepata maambukizi ya VVU kutokana na dalili na viashiria vyake hapa kufanana sana na dalili za magonjwa mengine. Mgonjwa aliye katika hatua hii ya kwanza ya maambukizi ya VVU huweza kuonesha dalili na viashiria kama vile kuvimba tezi (swollen lymph glands), kupatwa na homa kali, kuumwa koo (sore throat), kujihisi mchovu, kujihisi maumivu sehemu mbalimbali mwilini (body aches), kutokwa na vipele mwilini (skin rash), na pia kutapika, kuharisha au kuumwa tumbo
Mgonjwa anayepata dalili na viashiria hivi tunasema kwamba amepata Acute HIV infection/Acute HIV retroviral infection au seroconversion illness. Dalili hizi hutokana na mwili wa mtu mwenye maambukizi ya VVU kuanza kutengeneza kinga dhidhi ya VVU.
Hatua ya Pili (Clinically Asymptomatic Stage)
Katika hatua hii ambayo inaweza kudumu kwa muda wa miaka kumi, mgonjwa anakuwa haonyeshi dalili/viashiria vyovyote vile isipokuwa anaweza kuwa na tezi zilizovimba [swollen lymph nodes]. Kiwango cha VVU kwenye damu hupungua sana lakini mgonjwa anaweza kuambukiza mtu mwingine yoyote na vipimo vya VVU vina uwezo wa kutambua uwepo wa maambukizi y VVU katika damu.
Tafiti mablimbali zimeonesha kwamba VVU katika mwili huwa bado zinazaliana [active] na hukimbilia/hujificha kwenye tezi [lymph nodes]. Kutokana na kujificha kwake katika hatua hii, kipimo cha kupima wingi wa virusi vya ukimwi (Viral load test) katika mwili hutumiwa sana ili kuweza kutambua uwepo wa VVU. Kipimo hiki pia husaidia katika kumpangia mgonjwa tiba yake.
Hatua ya Tatu [Symptomatic HIV infection]
Kutokana na kuongezeka kwa wingi wa VVU katika mwili, kinga ya mwili huzidi kudhoofika na hii husababishwa na;
Tezi na tishu zilizoathiriwa na VVU huharibika kutokana na maambukizi ya muda mrefu
VVU hubadilika badilika na kuwa na uwezo zaidi wa kuathiri tishu na sehemu mbalimbali za mwili na hata kuziua/kuziharibu seli zinazokinga mwili kutokana na maambukizi zinazojulikana kama T helper cell
Mwili hushindwa kumudu uharibifu wa T helper cell na kushindwa kuzalisha seli nyingine mpya.
Dawa za kuvubaisha VVU au Antiretroviral therapy huanza kutumiwa wakati seli aina ya CD4 zinapopungua na kuwa kiwango cha chini sana. Kupungua kwa seli hizi za CD4 ni kielelezo cha kinga ya mwili kuwa dhaifu. Matumizi ya dawa hizi huboresha kinga ya mwili na kumfanya mgonjwa kuishi kwa muda mrefu bila kuonyesha dalili au viashiria vyovyote vile [yaani kumrudisha mgonjwa katika hatua ya pili].
Kama mgonjwa wa VVU hatumii dawa za kuvubaisha VVU au anatumia ARV's ambazo hazimsaidii au hazifanyi kazi vizuri mwilini mwake, basi mgonjwa ataendelea kuingia kwenye hatua ya nne ya Ukosefu wa Kinga Mwilini (Ukimwi) au AIDS.
Hatua ya Nne [UKIMWI]
Kama nilivyoeleza hapo juu, hatua hii hujulikana kama Ukosefu wa Kinga Mwilini [UKIMWI] au AIDS, ambapo mgonjwa hupata maambukizi ya magonjwa nyemelezi pamoja na saratani za aina mbalimbali kutokana na kupungua kwa kinga mwilini.
Vigezo vilivyopangwa na shirika la afya duniani (WHO) ili kuweza kutambua kama mgonjwa yupo kwenye hatua hii ya UKIMWI hutofautiana kati ya watu wakubwa na watoto chini ya miaka 5. Pamoja na kuwa WHO wameweka vigezo vya pamoja, utambuzi wa hatua za ugonjwa wa UKIMWI hutofautiana kati ya nchi na nchi kutokana na miongozo tofauti ya nchi hizo.
Kwa watu wazima na watoto walio na umri zaidi ya miaka mitano, uwepo wa ugonjwa wowote nyemelezi pamoja na kushuka kiwango cha CD4 chini ya 200 cells/mm3 au kushuka kwa seli za CD4 chini ya asilimia 15 hutambulika kama ugonjwa wa UKIMWI.
Kwa watoto walio chini ya miaka mitano, uwepo wa ugonjwa wowote nyemelezi/kushuka kwa seli za CD4 chini ya asilimia 20 [kwa wale wenye umri kati ya miezi 12-35] hutambulika kama wana ugonjwa wa UKIMWI.
Watoto wenye umri chini ya miezi 12, kupungua kwa seli za CD4 chini ya asilimia 25 ndiyo hutumika kutambulisha wana ugonjwa wa UKIMWI.
CD4 ni nini?
CD4 ni aina ya protini inayopatikana katika ukuta wa seli zinazojulikana kama T helper cell [pia hujulikana kama CD + lymphocyte]. VVU hushambulia na kujishikiza kwenye protini hii kabla ya kupata uwezo wa kuathiri seli za T helper cell. Seli hizi za T helper cell ndizo hulinda mwili dhidi ya maambukizi mbalimbali na hivyo kuchangia katika kustawi kwa kinga ya mwili. Kupungua kwa seli hizi mwilini husababisha kupungua kwa kinga ya mwili na hivyo mtu kupata magonjwa mbalimbali.
Magonjwa nyemelezi/saratani (opportunistic infections/cancer)
Baadhi ya magonjwa nyemelezi yanayoweza kumpata mtu mwenye ugonjwa VVU/UKIMWI ni pamoja na
a. magonjwa ya mfumo wa kupumua kama vileugonjwa wa homa ya mapafu (pneumocyctic carinii pneumonia), Kifua kikuu (TB) na Kaposis sarcoma (saratani);
b. Magonjwa ya mfumo wa chakula kama vile Cryptosporidiosis, Candida (fangasi), Cytomegolavirus (CMV), Isosporiasis, na Kaposi's Sarcoma
c. Magonjwa ya mfumo wa fahamu (Central/peripheral nervous system) kama vile Cytomegolavirus, Toxoplasmosis, Cryptococcosis, Non Hodgkin's lymphoma (saratani), Varicella Zoster (mkanda wa jeshi), Herpes simplex
d. Magonjwa mbalimbali ya ngozi [skin diseases] kama vile Herpes simplex, Kaposi's sarcoma (saratani ya ngozi) na Varicella Zoster [mkanda wa jeshi]
Hatua za VVU/UKIMWI kulingana na dalili za ugonjwa [clinical classification of HIV/AIDS]
Kutokana na uhaba wa vifaa vya kupimia kiwango cha seli aina ya CD4 katika nchi mbalimbali, shirika la afya duniani, limetengeza muongozo mwingine ambao utamsaidia mhudumu wa afya kuweza kutambua kama mgonjwa amefikia hatua ya ugonjwa wa UKIMWI na anastahili kuanza tiba au la. Uainishaji wa namna hii huitwa clinical classification of HIV/AIDS.
Hatua ya Kwanza [Clinical stage I]
Mgonjwa hana dalili zozote (asymptomatic)
Kuwepo kwa uvimbe katika tezi ambao hauondoki (persistant lymphadenopathy)
Hatua ya Pili [Cilinical stage II]
Kupungua uzito chini ya asilimia 10 ya uzito wa mwili bila sababu maalum
Magonjwa ya mara kwa mara kwenye mfumo wa upumuaji kama magonjwa ya masikio, kinywa, tezi la koo nk (sinusitis, tonsillitis, otitis media, pharyngitis)
Mkanda wa jeshi (Herpes zoster)
Vidonda pembezoni mwa mdomo (Angular chelitis)
Vidonda vya mara kwa mara kwenye kinywa (Recurrent oral ulceration)
Vipele mwilini (Papular pruritic eruptions)
Ugonjwa wa ngozi [Seborrhoeic dermatitis]
Maambukizi ya fangasi katika kucha [Fungal nail infections]
Hatua ya Tatu [Clinical stage III]
Kupungua uzito kwa zaidi ya asilimia 10 ya uzito wa mwili bila sababu yoyote maalum
Kuharisha zaidi ya mwezi mmoja bila sababu yoyote maalum
Kuwa na homa isiyoelezeka [homa hii inaweza kuwa inapona na kujirudia au homa ambayo inakuwepo kwa zaidi ya mwezi mmoja]
Maambukizi ya fangasi kwenye kinywa [Persistent oral candiadiasis]
Oral hairy leukoplakia
Ugonjwa wa kifua kikuu kwenye mapafu [kwenye mapafu]
Maambukizi hatari ya vimelea vya bakteria [homa ya mapafu, ugonjwa wa uti wa mgongo, maambukizi katika mifupa na jointi, empyema, pyomyositis, bacteraemia]
Maambukizi hatari kwenye kinywa [Acute necrotizing ulcerative stomatitis, gingivitis or periodontitis]
Upungufu wa damu mwilini bila sababu yoyote maalum [Unexplained anaemia (below 8 g/dl), neutropenia (below 0.5 billion/l) and/or chronic thrombocytopenia (below 50 billion/l)]
Hatua ya Nne (Clinical stage IV)
Kudhoofika mwili [HIV wasting syndrome]
Homa kali sana ya mapafu [Pneumocystis pneumonia]
Saratani ya shingo ya kizazi [invasive cervical cancer]
Homa kali sana ya mapafu inayojirudia inaosababishwa na vimelea vya bakteria
Magonjwa ya kwenye mfumo wa figo/moyo yayochangiwa na VVU [Symptomatic HIV-associated nephropathy or HIV-associated cardiomyopathy]
Maambukizi ya fangasi katika mishipa ya kupitisha chakula mpaka kwenye mapafu na mishipa yake ya kupitisha/kusambaza hewa mwilini
Ugonjwa wa kifua kikuu uliosambaa mwilini [disseminated mycobacteria tuberculosis]
Maambukizi ya fangasi yaliyosambaa mwilini [histoplasmosis, coccidiomycosis]
Saratani ya kwenye tishu za mwili [kaposis sarcoma]
Maambukizi kwenye mishipa ya fahamu yanayosababishwa na vimelea aina ya toxoplasma gondii [Central nervous system toxoplasmosis]
Maambukizi ya VVU kwenye ubongo na kusababisha mgonjwa kuwa kama mgonjwa wa akili [HIV encephalopathy]
Ugonjwa wa uti wa mgongo uliosambaa mwilini [Extrapulmonary cryptococcosis including meningitis]
Ugonjwa wa kifua kikuu uliosambaa mwilini ambao hausababishwi na vimelea aina ya mycobacteria tuberculosis [Disseminated non-tuberculous mycobacteria infection]
Aina ya ugonjwa unaoathiri ubongo na kumfanya mgonjwa shindwe kufikiri sawasawa [Progressive multifocal leukoencephalopathy]
Chronic cryptosporidiosis na Chronic isosporiasis
Recurrent septicaemia [including non-typhoidal Salmonella]
Lymphoma [cerebral or B cell non-Hodgkin]
Atypical disseminated leishmaniasis
Cytomegalovirus infection [retinitis or infection of other organs]
Chronic herpes simplex infection [orolabial, genital or anorectal of more than one months duration or visceral at any site].