Nani anasema Pep Guardiola ndiye kocha bora? Vipi kuhusu Zidane?



Ufundi wa hali ya juu wa gwiji wa Real Madrid ulimaliza ubishi na mijadala yote juu ya uwezo wa Zinedine Zidane baada ya ushindi dhidi ya Atletico Madrid katika dimba la Vicente Calderon Jumamosi usiku, mechi ambayo Simeone alizidiwa kila kitu.

Cha kushangaza pamoja na kwamba aliweza kushinda Undecima, UEFA Super Cup na kucheza mechi 28 bila kupoteza – mafanikio haya yalionekana hayatoshi, kwa sababu wengi walikuwa wanaamini timu ilikuwa haichezi vyema na ilikuwa inatembea mwendo wa kubahatisha.

Alikuwa na majeruhi wengi kabla ya mechi hiyo kubwa ya jiji la Madrid, lakini uendeshaji mzuri wa kikosi ulimaanisha hata wachezaji ambao hawakuwa wakipata nafasi ya kucheza, walikuwa na utayari wa kutoa mchango wao kwenye kikosi – hasa Isco.

Zidane pia ameonyesha kuwa mbunifu kimbinu, akitumia mfumo wa 4-2-3-1 Isco akicheza nyuma ya Cristiano Ronaldo mfumo ambao umekuwa na tija kwenye kikosi cha Los Blancos na hata kuwashangaza Atletico Madrid.

Zidane pia amekuwa akihamia kwenye mfumo wake wa kawaida 4-3-3 na 4-4-2 kulingana na wachezaji alionao, na unyambulifu huu wa mbinu umekuwa mzuri kwenye kikosi chake.
Baada ya mechi 32, Zidane amefanikiwa kupata pointi 83, mbili zaidi ya Pep Guardiola alizofanikiwa kupata wakati akiwa na kikosi bora cha Barcelona.

Ameshinda mechi 26, sare 5 na amepoteza mchezo mmoja tu, na baada ya kukosa ubingwa wa La Liga kwa muda mrefu, hiki ni kipaumbele na Zidane ndio mtu wa kufanikisha.

Je! Barcelona wanaweza kuleta upinzani wa kutisha kiasi cha kuitoa Real Madrid kwenye reli ya kuwania ubingwa wa La Liga msimu huu?

Real Madrid wakiendelea kwa mwendo thabiti, bila shaka wanaweza kubakiza tena kikombe cha Ligi ya Mabingwa Ulaya, Uefa.