Wakili aomba radhi kwa kushindwa kumkamata Tundu Lissu

Wakili wa Serikali, Patrick Mwita amemuomba radhi Hakimu Mkazi Mkuu wa Kisutu kwa kushindwa kutekeleza amri ya kumkamata mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anayekabiliwa na kesi ya uchochezi pamoja na wahariri wa gazeti la Mawio.

Wakili Mwita alifanya hivyo jana baada ya hakimu huyo, Thomas Simba kumuhoji sababu za kushindwa kutekeleza amri hiyo wakati hati ya kumkamata ilitolewa Novemba 3, 2016 na wakili huyo kuisaini. “Kwa nini hamkumkamata” Si mlikuwa na wajibu wa kumkamata? Mnamuogopa?” alihoji hakimu huyo.

Hata hivyo, pamoja na kuomba radhi hiyo mahakama imechukua hati ya kusafiria ya Lissu ili kudhibiti safari zake nje ya nchi kwa kuwa amekuwa akisafiri bila kuitaarifu mahakama.

Katika kesi hiyo, Lissu na watu wengine watatu wameshtakiwa kwa makosa matano ya uchocheza kutokana na habari iliyochapishwa na gazeti la Mawio kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 28, 2016 na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.

Kabla ya uamuzi huo, Wakili Mwita alisema jana ilikuwa siku ya kesi hiyo kutajwa na kwamba upelelezi unakaribia kukamilika.

Kuhusu madai ya kudharau mahakama Wakili Peter Kibatala anayemwakilisha Lissu aliiambia mahakama kuwa mteja wake yupo mahakamani, hivyo ametii amri ya mahakama na kwamba jukumu la dhamana ni kuhakikisha mshtakiwa anakuwapo mahakamani wakati wa kesi yake na kwamba uwepo wake ni kutii masharti ya dhamana.

Hata hivyo, Wakili Mwita alidai kuwa kitendo cha Lissu kutofika mahakamani mara mbili mfululizo ni kama kuonyesha dharau kwa mahakama hiyo.

Mwita alidai kuwa Lissu ni mwanataaluma wa sheria na anafahamu taratibu za kufuatwa kama hafiki mahakamani na kwamba mdhamini si mbadala wa mshtakiwa mahakamani. “Alipaswa kuandika barua kuitaarifu mahakama hii kama wakili kuwa ana kesi ya uchaguzi anayoiendesha Bunda na kuambatanisha na samansi ama orodha ya kesi. Tunaomba mahakama iheshimiwe na jukumu la kumfutia dhamana ama kutokumfutia dhamana Lissu bado lipo mikononi mwako mheshimiwa,” alieleza wakili huyo wa Serikali. #Mwananchi