Wafugaji 50 Wala Kinyesi, Damu na Mkojo Kunusuru Maisha Yao ,wapotea ndani ya Pori la Akiba la Selous
Watu 50 wakiwa na watoto wadogo wamenusurika kufa, baada ya kupotea ndani ya Pori la Akiba la Selous kwa siku saba; huku wakikosa chakula na maji na kulazimika kula kinyesi cha ng’ombe, damu na mikojo ya binadamu.
Watu hao ambao ni wafugaji, walikuwa wakihama na mifugo yao inayokadiriwa kufikia 1,780 kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, yakiwemo Chumvi na Muhoro waliekea Morogoro, ambako walidai ndiko yalipo makazi yao.
Tukio hilo ambalo si la kawaida kutokea katika pori hilo, lilianzia Jumatano iliyopita wakati wafugaji hao, walipoanza safari ya kuelekea Malinyi mkoani Morogoro, wakiongozwa na mwenyeji wao, waliyemtaja kwa jina la Mzee Mzigua, ambaye hata hivyo wanadai aliwalaghai na kuwatelekeza.
Wafugaji hao walisema walitembea kwa siku tano ndani ya pori hilo, wakitarajia kufika Malinyi, yaliko makazi yao. Lakini hali ilikuwa tofauti, baada ya mwenyeji wao huyo, kuwalaghai kwa kuwapitisha njia sisizo sahihi.
Walisema waliishiwa chakula na maji ya akiba na mwisho walijikuta wanatokea ndani ya Pori la Akiba la Selous; huku hali zao zikiwa zimedhoofu kutokana na njaa na kiu cha maji. Wakiwa safarini, mwenyeji wao huyo, aliwataka kila mmoja alipe fedha ikiwa ni ujira wake kwa kuwaonyesha njia. Walidai kuwa walimlipa fedha nyingi.
Wengine walimlipa Sh milioni mbili, Sh milioni moja na wengine Sh 500,000, wakitarajia angewasaidia. Walitembea usiku na mchana ndani ya pori hilo, wakipishana na wanyama wakali kama simba na nyati, hivyo kuhatarisha usalama wa maisha yao na watoto wao.
Hali ilizidi kuwa mbaya zaidi, baada ya kutimia siku ya tano wakiwa ndani ya pori hilo, pale walipoishiwa chakula na maji, hivyo kuwalazimu kuanza kuchinja ng’ombe na kunywa damu kwaajili ya kukata kiu. Pia walikula kinyesi chao ili kupunguza njaa. Yule mwenyeji wao aliwatelekeza baada ya kuona hali zao zimekuwa mbaya.
Alitokomea kusikojulikana, akiwaacha wasijue pa kwenda, hivyo kulazimika kutelekeza mifugo yao ili kunusuru kwanza maisha yao. Halikadhalika, wengine walilazimika kunywa mikojo yao na mingine kuwanywesha watoto wao kunusuru maisha yao, hali iliyowafanya kuathirika kiafya na kushindwa kuendelea na safari.
Wengine walianguka na kupoteza fahamu. “Sisi tulikuwa tunataka turudi nyumbani kwetu Morogoro. Huku tulikuja wakati wa operesheni ya Morogoro, huku tulikuja kununua ng’ombe lakini miji yetu ipo kule Morogoro. Tukaambatana na huyo mwenyeji wetu aliyejitambulisha kwa jina la Mzee Mzigua na mtoto wake.Lakini tunajua mpaka nyumbani kwake”alisema Kiongozi wa msafara wa wafugaji hao, aliyejitambulisha kwa jina la Lisesi Cherahani Bela na kuendelea;
“Zilitimia kama siku nne tukiwa hatujanywa maji, jua lilikuwa linawaka, tukaanza kuanguka, tukaanza kuchinja ng’ombe na kunywa damu, tulijaribisha kula kinyesi cha ng’ombe, tulikuwa tunakojoa mkojo tunanywesha hata watoto. Mimi nilikunywa mkojo lita moja, ikaniathiri hapa kifuani, kumbe mkojo ni kitu kibaya.”
Akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika eneo hilo, kiongozi huyo alisema baada ya kuona hali inakuwa mbaya zaidi, alitafuta eneo ambalo lina mtandao wa simu na kufanya mawasiliano na watu mbalimbali, ambapo alifanikiwa kuwasiliana na watu wa Kigoma na kuomba msaada wao.
Alisema kuwa watu hao, waliwasiliana na wahifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na kuwasiliana na wahifadhi wa Pori hilo la Selous, ambao walianza kazi ya kuwasaka na hatimaye kuwakuta katika eneo la Mlima Luhombelo, lililopo katikati ya Pori hilo wakiwa tayari wameshadhoofika kiafya.
Askari hao wa wanyamapori wa Pori hilo, waliwapatia uji na maji na kuwapa huduma ya kwanza wale wengine ambao walikuwa na hali mbaya.
Baada ya taarifa hizo za kupotea kwa wafugaji hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Gaudence Milanzi alifika katika eneo hilo juzi, akiambatana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Martin Leibooki, Meneja wa Pori la Akiba la Selous, Henock Msocha na maofisa wengine wa wizara na pori hilo.
Milanzi alisema Serikali inaangalia namna ya kuwasaidia wafugaji hao, kurejea katika hali zao kiafya pamoja na kuwasaidia kutafuta mifugo yao ili waweze kurejea katika makazi yao na kuendelea na shughuli zao.
“Kwa upande wa Serikali kama Wizara hatuchukulii kama hawa wameingia kwenye hifadhi hapana, muhimu kwanza ni kuokoa maisha ya binadamu, na hicho ndicho tunategemea kukifanya sasa hivi, na baada ya hapo kutakuwa na masuala ya kutafuta hiyo mifugo, kwa sababu wamepata hasara kubwa”alisema Katibu Mkuu huyo.
Aliutaka uongozi wa wilaya ya Rufiji, kutoa ushirikiano na wizara ili kuwabaini waliowadanganya wafugaji hao, kwa kuwaingiza kwenye pori hilo na kuwatapeli kiasi hicho kikubwa cha fedha.
“Hawa waliowadanganya na kupita huko ndani ya pori kwa kweli tutaendelea kuwatafuta na tutaomba tuwe na ushirikiano na uongozi wa Wilaya kwa sababu inaelekea kuna watu kazi yao ndo hiyo, ukiangalia pesa walizowapa ni nyingi sana, sasa watu wamechukua pesa zote na wamewaacha katika hali kama hii, wengine wana watoto wadogo, kwa hiyo tutahakikisha tunashirikiana kuwatafuta ili tukomeshe hili tatizo moja kwa moja”alisema.
Katibu Mkuu huyo alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TAWA na Mhifadhi Selous kwa juhudi za haraka walizochukua. Alisema wizara yake itaendelea kushirikiana na Mamlaka mbalimbali, kutoa misaada ya haraka, endapo yatatokea tena matukio ya aina hiyo.
Kwa upande wake, Leibooki alisema TAWA ambao ndiyo wamiliki wa hifadhi zote za wanyamapori nchini, haitawachukulia hatua za kisheria wafugaji hao, kwa kuwa waliingia ndani ya pori kwa kudanganywa na watu wenye nia mbaya.
Lakini, alisisitiza kuwa mamlaka yake, itawashughulikia kisheria wawindaji haramu na wafugaji wanaoingiza mifugo yao ndani ya hifadhi zilizo chini ya Mamlaka yake.
Pia alisema Mamlaka yake, inaendelea na utaratibu wa kushirikiana na wananchi waishio pembezeni mwa hifadhi zote, kwa kuwapa elimu ya ufugaji bora kwa kushirikiana na wizara zinazohusika na kuendeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo miundombinu ya maji.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafugaji chini (CCWT), Magembe Makoye aliwataka viongozi wa Halmashauri mbalimbali nchini, kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji mahali walipo, bila ya kuondoa watu wengine.
Alisema kuwa wao kama chama, wamesikitishwa na tukio la kuondolewa kwa wafugaji hao katika bonde hilo la Rufiji, kwa kuwaambia warudi walipotoka. Alisema tamko hilo lilitolewa na uongozi wa Halmashauri hiyo na ndilo lililosababisha matatizo hayo.
Makoye alisema kufanya hivyo, hakuondoi migogoro ya wafugaji na wakulima, badala yake ni kuendelea kuzalisha migogoro hiyo katika maeneo mengine, ambayo wafugaji watahamia.
“Tunalaani kweli vitendo hivi vya viongozi na watendaji wengine wa Halmashauri kuwafukuza wafugaji, tena wakati mwingine kwa kuwatisha na matokeo yake wananchi hawa 50 wangepoteza maisha, kama isingekuwa bahati ya mtu mmoja kuwa na simu kati yao” alisema Katibu Mkuu huyo.
“Kwa kweli kwa niaba ya wafugaji wote wa Tanzania naishukuru sana Wizara ya Maliasili kupitia kwa Katibu Mkuu, Gaudence Milanzi.”alisema Katibu huyo.
Alisema kuwa kungeweza kutokea majanga makubwa zaidi kwa kuwa kuwa wafugaji hao walikuwa wakisafiri na watoto wao wadogo katika mazingira hatarishi katikati ya pori hilo, ambalo lina wanyama wakali.
“Kwa kweli ni mazingira ya kusikitisha. Lakini niishukuru sana Serikali kwa maana ya Wizara ya Maliasili na Utalii, wamefanya kazi yao kwa namna ambavyo mimi ninawiwa kuwashukuru. Tangu jana tumewasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara, leo watu wote wameweza kupatikana, kumefanyika doria ya ndege, doria za magari, doria kwa miguu, wamewatafuta hawa watu, wamewaokoa, wamewaleta kwenye huduma za afya, wamewapa chakula, wamewahifadhi, hawajawadhuru”alisema.
Aliiomba Serikali kuhakikisha tatizo la wafugaji nchini, linatafutiwa ufumbuzi wa kudumu, kwani jamii haiwezi kuendelea kubaki na tatizo hilo kwa miaka yote. Alitaka wafugaji watafutiwe maeneo ya kudumu ya kufugia, ikiwa ni pamoja na kupimiwa maeneo yao, badala ya hali ilivyo sasa kuafukuza kila kukicha.