Kimenuka..CUF ya Maalim Seif Yatoa Majibu Haya kwa Prof Lipumba..!!!

Chama cha Wananchi (CUF) kimesema hakitafanya mazungumzo kusaka suluhu na mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na msajili wa vyama vya siasa na kwamba, kipo tayari kwa lolote hata kama kitafutiwa usajili.

Pia, chama hicho kimesema hakijuti kumkaribisha na kumuunga mkono Edward Lowassa, ambaye aliteuliwa kugombea urais mwaka 2015 kwa tiketi ya Chadema na kuwakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Maelezo hayo yalitolewa juzi na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Mbarala Maharagande kujibu madai yaliyotolewa na Profesa Lipumba alipohojiwa katika kipindi cha Funguka kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Azam.

Katika mahojiano hayo, Profesa Lipumba alidai kuwa mgogoro uliopo ndani ya chama hicho kwa sasa hautamalizwa na mahakama pekee bali viongozi wa pande mbili na kuzungumza, lakini Maharagande amesema haiwezekani kwa vile Lipumba alishakwisha kukivuruga na hafai tena kuendelea kuwa kiongozi.

“Lipumba anasema tukae tulimalize suala hili kwa kuongea sisi wenyewe. Jambo hilo haliwezekani kwa kuwa kama kupandikiza chuki, uhasama, uharibifu wa chama miongoni mwa wanachama na viongozi ameshafanya na kufanikiwa hilo kwa baadhi ya wanachama na viongozi wake na kuharibu taswira ya chama kwa jamii,” alisema Maharagande.