Njia 6 za Kufanikiwa alizozitaja Barack Obama




Obama si mchoyo, amekuwa akizungumza katika vituo mbalimbali vya televisheni na hata kwenye majukwaa kuwaeleza watu ni mambo gani wanatakiwa kufanya ili wafanikiwe.

Haya hapa chini ni miongoni mwa mambo hayo ambayo kama ukiyafanya, hakika utafanikiwa;


JUA UTAFANIKIWA TU.
Kuhusu mafanikio, Obama anasema kama unataka kufanikiwa ni lazima ujue na kuamini kwamba utafanikiwa tu.
Wengine wamekuwa hawafanikiwi kwa kuwa hawajui kama watafanikiwa. Alitolea mfano hai kwamba mwaka 1962, aliyekuwa Rais wa Marekani, John Kennedy aliwaambia Wamarekani kwamba hawawezi kwenda mwezini kwa kuwa ni mbali sana.

Lakini miaka saba baadaye Neil Armstrong akawa mwanadamu wa kwanza kufika huko. Hivyo ndiyo ilivyo, wengine wameambiwa maneno mabaya kwamba hawawezi kufika kwenye mafanikio kwa sababu tu wanaambiwa kwamba ni vigumu, ndugu yangu, kuanzia leo jua kwamba utafanikiwa hata kama kutakuwa na watu wengi wakizungumza maneno ya kukukatisha tamaa.

HUTAKIWI KURIDHIKA.
Obama anaendelea kusema kwamba ili ufanikiwe, hutakiwi kuridhika hata kidogo. Wengine wamekuwa wakianguka au kutokufanikiwa kwa kuwa tu waliridhika, waliingiza kiasi fulani cha fedha, wakajenga nyumba na kununua magari wakaridhika.

Mafanikio si kununua gari tu, si kununua nyumba tu, bali ni kuwa na biashara nyingi ambazo zitakuingizia fedha kila siku.


UWE NA MALENGO.
Obama anasema kuwa, huwezi kufanikiwa bila kuwa na malengo. Ni lazima unapoianza safari yako ujiwekee malengo kwani utakuwa ukifanya vitu kuendana na malengo uliyojiwekea.
Kama hutaweka malengo, utakuwa unafanya vitu bila mpangilio wala mwelekeo. Maisha ya mfanyabiashara ni lazima yawe na malengo ambayo ndiyo ramani ya biashara yako na mafanikio yako kwa jumla.


HUWEZI KUFANYA PEKE YAKO.
Kwa mujibu wa Obama kama walivyo wengine wote wenye mafanikio, safari ya mafanikio ni ndefu. Wengine wamekuwa wakihisi kwamba wanaweza kusimama wakiwa peke peke yao.

Ndugu zangu anachokisema Obama ni ukweli, huwezi kusimama peke yako hasa kwenye masuala ya biashara na ndiyo maana mara kwa mara unasikia kuna vikao vya wafanyabiashara. Utakapofanya kila kitu peke yako, hutapata mawazo mapya kwa sababu utakuwa unaiamini akili yako pekee katika kukufikisha sehemu f’lani.

Ili ufanikiwe, unatakiwa kuwashirikisha wafanyabiashara wenzako na ikiwezekana, ukianzisha jambo, unaweza kuwaita na kuhitaji ushauri wao, watakuwa msaada mkubwa kwako.




ACHA VISINGIZO.
Anasema kuwa wafanyabiashara wengine wamekuwa na kawaida ya kulalamika hovyo. Wanaanzisha malengo yao, lakini mwisho wa siku wanakuja na visingizio kwamba hawakufanikiwa kwa sababu fulani, hawakufanikiwa kwa kuwa kulikuwa na watu waliowavuta nyuma kutoka kule walipokuwa wakielekea.

Mfanyabiashara ukianza kutafuta visingizio, hutafika kwa sababu hakuna mfanyabishara anayefanya biashara bila kupitia vikwazo mbalimbali ambavyo usipokuwa makini ndivyo vitakavyokuwa visingizio. Kwamba, hujafanikiwa kwa kuwa haukuwa na muda mrefu wa kazi au visingizio vingine.

Unachokipata, kifanye tena kwa umakini mkubwa na kujitolea, achana na visingizio.

IFANYE BIASHARA YAKO IWE SERIOUS.
Obama anasema kwenye biashara kuna watu wanahisi kwamba wakiwa serious mno ndiyo wanaweza kufanikiwa. Huwezi kufanikiwa kama utayafanya maisha yako kuwa serious.

Matajiri wengi wanakuwa serious kwenye biashara na si maisha yao binafsi ndiyo maana wanacheka na watu, wanataniana ili maisha yasonge lakini kwenye biashara, huko ndipo unapotakiwa kuleta u-serious kupita kawaida, kwani ukileta utani, utafeli.